Libya: Misri, Saudia, Imarati zinavunja azimio la Baraza la Usalama
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58010-libya_misri_saudia_imarati_zinavunja_azimio_la_baraza_la_usalama
Mwakilishi wa serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, nchi za Misri, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) zinavunja azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa uungaji mkono wao kwa jenerali muasi, Khalifa Haftar.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Dec 20, 2019 23:34 UTC
  • Libya: Misri, Saudia, Imarati zinavunja azimio la Baraza la Usalama

Mwakilishi wa serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, nchi za Misri, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) zinavunja azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa uungaji mkono wao kwa jenerali muasi, Khalifa Haftar.

Shirika la habari la IRIB limeinukuu ofisi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya katika Umoja wa Mataifa ikisema hayo usiku wa kuamkia leo Jumamosi na kuongeza kwamba, licha ya kuwa maazimio ya Baraza la Usalama yanahimiza kutotumwa silaha nchini Libya, lakini nchi za Misri, Saudia na Imarati zinakanyaga azimio hilo na zinamsaidia kikamilifu jenerali muasi Khalifa Haftar, kwa silaha na fedha, na hivyo kuharibu utulivu na usalama wa Libya.

Amma kuhusiana na makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni baina ya serikali hiyo na Uturuki kuhusu mipaka ya majini, ofisi hiyo imesema, makubaliano na Uturuki hayakinzani na makubaliano ya kisiasa ya Libya na hayahitajii idhini ya pande nyingine.

Jenerali muasi Khalifa Haftar katika mazungumzo na mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin Abdulaziz

 

Itakumbukwa kuwa serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya iliundwa katika makubaliano baina ya pande mbalimbali za Libya yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa na kutiwa saini katika mji wa  Skhirat, Morocco, tarehe 17 Disemba 2015. Serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inaongozwa na Waziri Mkuu, Fayez al Sarraj.

Hata hivyo baadhi ya nchi hasa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri na baadhi ya nchi za Magharibi hadi leo zinaendesha kampeni za kufelisha juhudi za kuleta amani na utulivu huko Libya. Nchi hizo zinamuunga mkono jenerali muasi Khalifa Haftar anayeongoza kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya ambaye anadhibiti eneo la mashariki mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.