Uturuki yaonya kuhusu hatari ya Libya kugeuka kuwa Syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu, ambaye nchi yake inajitayarisha kutuma wanajeshi Libya ameonya kuwa, kuendelea mgogoro wa Libya kwa muda mrefu kunaweza kuitumbukiza nchi hiyo katika hali mbaya zaidi na kuigeuza kuwa sawa na Syria.
Akizungumza katika kikao cha chama tawala cha AK mjini Ankara, Cavusoglu amesema: "Iwapo leo Libya itageuka na kuwa kama Syria, basi nchi zingine katika eneo pia zitakumbwa na hatima sawa na hiyo."
Amengeza kuwa: "Kuna haja ya kufanya kila linalowezekana kuizuia Libya kugawanywa vipande vipande na kwa msingi huo tumechukua hatua." Aidha amesema katika kutuma wanajeshi Libya, Uturuki inashirikiana na serikali halali ya nchi hiyo ambayo inatambuliwa kimataifa.
Mwezi Novemba, Uturuki na Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya zilitiliana saini mapatano ya ushirikiano wa kiusalama na kijeshi. Kwa mujibu wa mapatano hayo, Uturuki inaweza kutuma askari Libya ikiombwa rasmi na serikali ya Tripoli.
Siku ya Alhamisi, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki alisema nchi yake imepokea ombi rasmi la kutuma askari Libya na kwamba askari hao watatumwa katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini baada ya Bunge la Uturuki kutoa idhini rasmi.
Tokea mwezi Aprili mwaka huu, serikali ya Libya imekuwa ikikabiliana na wanamgambo wanaoongozwa na jenerali Muasi Khalifa Haftar ambaye anapata uungaji mkono wa kifedha na kisilaha kutoka Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Libya ilitumbukia katika vita vya ndani tokea mwaka 2011 wakati Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) lilipoteka harakati ya wananchi na kumpindua na kisha kumuua dikteta wa zamani wa nchi hiyo Muammar Gaddafi.