Magaidi 33 wa kundi la al-Shabab waangamizwa nchini Somalia
(last modified Sat, 04 Jan 2020 13:34:21 GMT )
Jan 04, 2020 13:34 UTC
  • Magaidi 33 wa kundi la al-Shabab waangamizwa nchini Somalia

Wanamgambo wasiopungua 33 wa kundi la kigaidi la al-Shabab wameangamizwa katika operesheni mbili tofauti za jeshi kusini magharibi mwa Somalia.

Ismail Mukhtar Orongo, msemaji wa serikali ya Somalia amethibitisha kuuawa idadi hiyo ya wanamgambo wa al-Shabab na kubainisha kwamba, waliuawa jana katika operesheni mbili tofauti za jeshi la nchi hiyo.

Taarifa ya jeshi la Somalia imeeleza kuwa, makumi ya wapiganaji wa kundi hilo la kigaidi la al-Shabab wamejeruhiwa pia katiika operesheni hizo za kijeshi.

Opereseni hizo mbili za jeshi la Somalia zimefanyika siku nne tu baada ya jeshi la nchi hiyo kutangaza kuwa, limewaua magaidi saba na kuwakomboa wanakijiji 7 pia katika moja ya vijiji vinavyodhibitiwa na wanamgambo hao.

Wanamgambo wa al-Shabab wa Somalia

Hivi karibuni kundi la kigaidi la al-Shabaab lilijitangaza kuhusika na shambulizi la bomu lililotokea mwishoni mwa wiki katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na kuua makumi ya watu na kujeruhi wengine wengi.

Genge la kigaidi la al Shabab liliundwa mwaka 2007 kwa shabaha ya kuipindua serikali kuu ya Somalia. Mwaka 2011 genge hilo la ukufurishaji lilitimuliwa katika maeneo mengi liliyokuwa linayadhibiti ukiwemo mji mkuu Mogadishu. Hata hivyo bado lina wafuasi wake katika vijiji vya mbali vya Somalia.

Tags