Jan 07, 2020 08:06 UTC
  • Watu 30 wauawa katika mripuko wa bomu nchini Nigeria

Kwa akali watu 30 wameuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea karibu na daraja lenye shughuli nyingi katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Modu Ali Said ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, mripuko huo wa bomu ulitokea jana jioni katika mji wa Gamboru mpakani na Cameroon, ambapo watu 35 pia walijeruhiwa.

Hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na mripuko huo, ingawaje kundi la kigaidi la Boko Haram na magenge mengine ya kitakfiri yenye mfungamano na Daesh yamekuwa wakifanya ukatili wa namna hii katika nchi za magharibi mwa Afrika.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, wanachama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) walisambaza mkanda wa video unaoonyesha mauaji ya kikatili ya watu 11 katika sikukuu ya Krismasi. Genge hilo lilidai kuwa liliwakata vichwa Wakristo 11 wa Nigeria katika video hiyo ya kipropaganda.

Wanachama wa Boko Haram wakiwa wamebeba bendera za Daesh

Kundi la kigaidi la Boko Haram ambalo lilianzisha hujuma zake mwaka 2009 nchini Nigeria, lilitangaza kuungana na genge la Daesh ambapo pia limeendelea kufuata nyayo zake katika kutenda jinai mbalimbali ndani na nje ya nchi hiyo.

Kundi hilo hadi sasa limeua watu zaidi ya elfu 20 huko Niger, Cameroon, Nigeria na Chad; na kupelekea wengine zaidi ya milioni mbili kuwa wakimbizi. 

Tags