Azimio la Baraza la Usalama la UN la kutamatisha vita Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59099-azimio_la_baraza_la_usalama_la_un_la_kutamatisha_vita_libya
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kulipigia kura azimio lenye vipengee 55 vinavyoainisha ramani ya njia ya kutamatisha kikamlifu vita na mapigano nchini Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 12, 2020 03:59 UTC
  • Azimio la Baraza la Usalama la UN la kutamatisha vita Libya

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kulipigia kura azimio lenye vipengee 55 vinavyoainisha ramani ya njia ya kutamatisha kikamlifu vita na mapigano nchini Libya.

Rasimu ya azimio hilo iliyotayarishwa na Uingereza inataka pande hasimu za kisiasa za Libya zijitolee kuunga mkono usitishaji vita wa kudumu, huku ikitaka kuheshimiwa vikwazo vya silaha vya UN dhidi ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ambavyo vimekuwa vikikiukwa mara kwa mara.

Aidha rasimu hiyo ambayo itapigiwa kura leo Jumatano inataka washiriki wa mkutano wa Berlin kuhusu amani ya Libya uliofanyika Januari 19 kujiepusha na uingiliaji wa mambo ya ndani ya Libya, mbali na kutaka kukomeshwa mienendo ya kutumiwa mamluki katika mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Hii katika hali ambayo, pande hasimu za Libya zimekubaliana kukutana katika duru mpya ya mazungumzo iliyopangwa kufanyika tarehe 18 ya mwezi huu wa Februari huko Geneva, Uswisi.

Jenerali muasi Khalifa Haftar (kushoto) na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj

Hivi karibuni Ghassan Salame, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya alitangaza kwamba, pande zinazozozana nchini Libya zimekubaliana na mpango wa kuundwa Kamati ya Pamoja ya kijeshi itakayofanya shughuli zake chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa kwa minajili ya kuzipatia ufumbuzi hitilafu zilizopo baina ya pande mbili katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Machafuko nchini Libya yalipamba moto kuanzia mwezi Aprili mwaka jana baada ya jenerali muasi Khalifa Haftar kuanzisha vita vikubwa vya pande zote dhidi ya mji mkuu Tripoli kwa nia ya kuinganusha serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Fayez al Sarraj na ambayo ndiyo inayotambuliwa na jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa.