UN: Mapigano ya ndani Libya yanaweza kugeuka kuwa vita vya kieneo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59456-un_mapigano_ya_ndani_libya_yanaweza_kugeuka_kuwa_vita_vya_kieneo
Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya ametahadharisha kuwa mapigano ya ndani nchini humo yanaweza kugeuka kuwa vita vya kieneo.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Feb 29, 2020 03:43 UTC
  • UN: Mapigano ya ndani Libya yanaweza kugeuka kuwa vita vya kieneo

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya ametahadharisha kuwa mapigano ya ndani nchini humo yanaweza kugeuka kuwa vita vya kieneo.

Ghassan Salame amesema, sababu ya kutoa indhari hiyo ni kujiingiza madola ya kigeni nchini humo.

Salame ameashiria kufeli kwa mazungumzo ya suluhu ya Geneva na kueleza kwamba: Kundi moja haliko tayari kutuma mwakilishi wake katika mazungumzo ya kutafuta suluhu ya kisiasa; na kundi jengine linatoa masharti ambayo ni magumu mno kuweza kutekelezeka kwa ajili ya kutatua mgogoro wa Libya.

Aidha mwakilishi huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya amekanusha madai ya kuwepo uingiliaji katika kuainisha wawakilishi wa jumbe zinazoshiriki katika mazungumzo ya Geneva ya kuutafutia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa Libya.

Baada ya duru kadhaa za mazungumzo yaliyofeli ya kutafuta suluhu, yakiwemo yale yaliyofanyika nchini Russia na Ujerumani, pande mbili zinazopigana nchini Libya zilitangaza tarehe 25 Februari kuwa haziko tayari kushiriki mazungumzo ya amani ya Geneva.

Fayez al-Sarraj (kulia) na Jenerali Khalifa Haftar

Itakumbukwa kuwa, tangu mwezi Aprili 2019 na kwa msaada na uungaji mkono wa baadhi ya nchi ikiwemo Misri na Imarati vikosi vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar vinavyojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) vimeanzisha hujuma na mashambulio dhidi ya mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli unaodhibitiwa na Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa (GNA), ambayo ndiyo inayotambuliwa kimataifa.

Hatua hiyo imekabiliwa na jibu la serikali hiyo inayoongozwa na Fayez al-Sarraj, na kupelekea kushadidi mapigano na machafuko ndani ya nchi hiyo.../