Feb 29, 2020 13:32 UTC
  • Makumi wauawa katika mapigano ya kikabila Ethiopia na Somalia

Watu wasiopungua 12 wameuawa katika mapigano mapya ya kikabila katika jimbo la Gambella, magharibi mwa Ethiopia.

Mkuu wa eneo hilo, Thomas Tut amesema mbali na watu 12 kuuawa na wengine 21 kujeruhiwa, maelfu ya wengine pia wamelazimika kukimbia makazi yao wakihofia kushambuliwa.

Amesema, "watu elfu saba wamelazimika kuwa wakimbizi, nyumba 400 zimeteketezwa moto na mifugo 300 imeibiwa katika machafuko hayo yaliyofanyika ndani ya siku chache zilizopita."

Aidha maafisa usalama wamewatia mbaroni watu sita wanaotuhumiwa kuhusika na kuchochea mapigano hayo ya kikabila ambayo hushuhudiwa mara kwa mara katika majimbo tofauti ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. 

Mwaka jana serikali ya Ethiopia ilitangaza habari ya kuwakamata watu 62 ambao walihusika katika kuchochea mapigano ya kikabila katika mkoa wa Benishangul baina ya makabila ya Gumuz na Amhara.

Wanajeshi wa Somalia; mapigano ya ndani nchini humo yanakwamisha juhudi za kupambana na kundi la kigaidi la al-Shabab.

Katika hatua nyingine, watu 11 wameuawa baada ya Jeshi la Somalia kupambana na wanamgambo wa kundi moja la wapiganaji katika kile kinachotajwa na Wasomali kuwa ni mapigano makali zaidi baada ya misuguano ya kisiasa inayoendelea kuikwamisha nchi hiyo katika dimbwi la ghasia na machafuko.

Mivutano ilianza jioni ya Alkhamisi baina ya Jeshi la Taifa la Somalia na wanamgambo wa kundi la Ahlu Sunnah Wal Jama’a (ASWJ) ambapo habari zaidi zinasema, viongozi kadhaa wa kundi hilo wamejisalimisha kwa serikali ya Mogadishu baada ya makabiliano hayo.

Tags