UN, lazima jinai za machafuko ya nchini Burundi zichunguzwe
Umoja wa Mataifa umetaka kuanza kuchunguzwa vitendo vya mauaji nchini Burundi.
Zeid Ra’ad Zeid Al-Hussein, kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binaadamu amesema kuwa, mauaji dhidi ya maafisa na viongozi wa jeshi nchini Burundi hayawezi kuachwa bila kuchunguzwa. Aidha ametaka kuanza uchunguzi wa kina kwa lengo la kubaini wahusika wa jinai hizo na hatimaye kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Zeid Ra’ad Zeid Al-Hussein amefafanua kuwa kwa mujibu wa ripoti zilizopo, asilimia kubwa ya jinai hizo zinafanywa na watu wanaobeba silaha wasiofahamika na kwamba, kushadidi vitendo vya ukatili nchini Burundi kumezidisha wasi wasi. Aidha kamishna huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binaadamu ameitaka serikali ya Bujumbura na wapinzani kukaa kwenye meza ya mazungumzo kwa lengo la kurejesha usalama nchini humo. Itafahamika kuwa, hivi karibuni Burundi imeshuhudia mauaji ya maafisa wa serikali na kadhalika viongozi wa kijeshi akiwemo Athanase Kararuza, mshauri wa kijeshi wa Makamu wa Rais Pierre Nkurunziza, suala ambalo limeifanya hali ya mambo nchini humo kuwa tete .