Wagombea 6 wa urais nchini Burundi waidhinishwa, 4 watemwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59676-wagombea_6_wa_urais_nchini_burundi_waidhinishwa_4_watemwa
Tume ya Uchaguzi nchini Burundi (CENI) imeidhinisha majina ya wagombea sita wa uchaguzi wa urais unaotazamiwa kufanyika mwezi Mei mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 11, 2020 07:44 UTC
  • Wagombea 6 wa urais nchini Burundi waidhinishwa, 4 watemwa

Tume ya Uchaguzi nchini Burundi (CENI) imeidhinisha majina ya wagombea sita wa uchaguzi wa urais unaotazamiwa kufanyika mwezi Mei mwaka huu.

Miongoni mwa wagombea walioidhinishwa na CENI ni Jenerali Evariste Ndayishimiye, Katibu Mkuu wa chama tawala cha CNDD-FDD na kinara wa chama kikuu cha upinzani nchini humo cha National Congress for Liberty (CNL) Agathon Rwasa; wawili hao wanatazamiwa kuchuana vikali kwenye uchaguzi huo.

Hata hivyo CENI imetupilia mbali faili la aliyekuwa rais wa Burundi katika kipindi cha mpito kati ya mwaka wa 2003 na 2005 Domitien Ndayizeye. Sababu za kukataliwa kwa ombi la kiongozi huyo wa muungano wa 'Kira Burundi' unaoundwa na vyama vidogo vidogo vya upinzani hazijajulikana.

Wagombea wengine ambao maombi yao ya kuwania urais nchini Burundi hayakuidhinishwa na Tume ya Uchaguzi CENI ni viongozi wa vyama vidogo vitatu vya siasa: Anicet Niyonkuru wa chama cha CDP, Jaques Bigirimana wa chama cha FNL na Valentin Kavakure wa chama cha FPN.

Agathon Rwasa kinara wa upinzani Burundi

Wagombea hao wana siku mbili za kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa Tume ya Uchaguzi katika Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo.

Wananchi wa Burundi wanatazamiwa kushiriki uchaguzi mkuu hapo tarehe 20 mwezi Mei mwaka huu kumchagua mrithi wa Rais Pierre Nkurunziza ambaye yuko madarakani tokea mwaka 2005.