"Wahajiri" 60 wapatikana wameaga dunia ndani ya lori Msumbiji
(last modified Thu, 26 Mar 2020 11:27:40 GMT )
Mar 26, 2020 11:27 UTC

Miili zaidi ya 60 imepatikana ndani ya lori la mizigo katika mkoa wa Tete, kaskazini magharibi mwa Msumbiji.

Makumi ya watu waliokuwa wamerundikana kwenye lori hilo wanadaiwa kuwa wahajiri kutoka Ethiopia. Habari zinasema kuwa, lori hilo lisimamishwa na maafisa wa polisi na uhamiaji katika mkoa wa Tete nchini Msumbiji, karibu na mipaka ya Malawi na Zimbabwe mapema Jumanne, likotokea Malawi.

Amelia Direito, msemaji wa Idara ya Uhamiaji ya mkoa wa Tete nchini Msumbiji amesema kuwa, walilisimamisha lori hilo baada ya kusikia sauti za watu wakiligonga kutoka ndani.

Amesema baada ya kulisimamisha lori hilo, walikuta maiti 64 na watu 14 ambao walikuwa hai. Amesema yumkini watu hao wanaodaiwa kuwa wahajiri waliaga dunia kwa kuishiwa na hewa.

Lori la jokofu lilikuwa na makumi ya miili Uingereza mwaka jana

Hii sio mara ya kwanza kwa wahajiri wa Kiafrika kupoteza maisha baada ya kukosa hewa wakiwa ndani ya malori wakisubiri kupelekwa kutafuta kazi na maisha mazuri barani Ulaya. Oktoba mwaka jana, miili 39 ya wahajiri wa Kiafrika ilipatikana ndani ya lori lililokuwa limeegeshwa katika eneo la Grey, jijini Essex, mashariki mwa London, kusini mashariki mwa Uingereza.

Wahamiaji wengi wamekuwa wakijaribu kuingia Ulaya katika miaka ya hivi karibuni kwa kujificha katika makasha ya malori au kwa usafiri hatarishi wa boti za plastiki.