Umoja wa Afrika walaani kitendo cha Marekani cha kuikatia misaada WHO
Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) amelaani kitendo cha Marekani cha kulikatia misaada ya kifedha Shirika la Afya Duniani (WHO) la Umoja wa Mataifa tena wakati huu wa vita vya dunia nzima dhidi ya corona.
Mwenyekiti huyo wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ameelezea kuhuzunishwa sana na hatua ya rais wa Marekani, Donald Trump ya kulikatia misaada ya kifedha shirika la WHO wakati huu ambapo dunia imezama katika vita dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 na kusisitiza kuwa, dunia hivi sasa inaihitajia mno WHO kuliko wakati mwingine wowote katika kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa corona.
Donald Trump analituhumu Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa linaipendelea China na anadai kuwa eti shirika hilo halikuitahadharisha Marekani kuhusu kirusi cha corona. Shirika la Afya Duniani (WHO) limekanusha madai hayo ya Trump kama ambavyo limesema halifanyi upendeleo wowote katika kazi zake.
Wakosoaji wa hatua hiyo ya Trump wamelaani vikali ubeberu huo wa Marekani na kusema kuwa, Trump anatafuta kisingizio tu cha kuhalalisha uzembe aliofanya wa kushindwa kukabiliana na maambukizi ya corona nchini Marekani.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres ameelezea kusikitishwa sana na hatua hiyo ya Trump ya kulikatia misaada ya kifedha Shirika la Afya Duniani ambalo liko chini ya umoja huo na kusema kuwa, hatua hiyo inakinzana na jitihada za kimataifa za kupambana na maambukizi makubwa ya corona.
Taasisi mbalimbali duniani ukiwemo Umoja wa Ulaya nazo zimelaani vikali hatua hiyo ya Donald Trump huku baadhi ya nchi zikiwa tayari zimeongeza kiwango cha misaada yao kwa WHO ili kuionesha Marekani kuwa hatua yake ya kulikatia misaada Shirika la Afya Dunia haiitalisambaratisha shirika hilo.