Watu wenye silaha wafanya hujuma mpya jijini Bujumbura Burundi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6040-watu_wenye_silaha_wafanya_hujuma_mpya_jijini_bujumbura_burundi
Watu wenye silaha wamefanya shambulizi huko Bujumbura, mji mkuu wa Burundi, na kuua na kujeruhi watu kadhaa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 29, 2016 11:42 UTC
  • Watu wenye silaha wafanya hujuma mpya jijini Bujumbura Burundi

Watu wenye silaha wamefanya shambulizi huko Bujumbura, mji mkuu wa Burundi, na kuua na kujeruhi watu kadhaa.

Polisi ya Burundi imetangaza leo kuwa, watu wanne wasiojuliokana walifanya shambulizi usiku uliopita katika eneo la Musaga, kusini mwa mji wa Bujumbura. Moïse Nkurunziza, naibu wa msemaji wa jeshi la polisi la Burundi amesema kuwa watu hao walianza kuwamiminia risasi watu waliokuwa wakijishughulisha na manunuzi katika eneo hilo la Musaga. Kwa mujibu wa jeshi hilo la polisi, katika hujuma hiyo, raia wanne na askari mmoja waliuawa huku watu wengine watatu wakijeruhiwa. Moïse Nkurunziza ameongeza kuwa, washambuliaji walitoroka kutoka katika eneo hilo kabla ya kufika askari wa serikali. Hayo yanajiri katika hali ambayo Pierre Claver Mbonimpa, mtetezi wa haki za binadamu nchini Burundi amewaambia waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani kwamba, waliouawa nchini Burundi hadi sasa ni watu 1,098 na kwamba wengine zaidi ya 800 hawajulikani waliko.