Jeshi la Libya lashambulia wanamgambo wa jenerali muasi Khalifa Haftar
Jeshi la Anga la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya ambayo inatambuliwa kimataifa limeshambulia basi moja lililokuwa limebeba wanagambo wa jenerali muasi Khalifa Haftar, kusini mwa Tripoli, mji mkuu wa nchi hiyo.
Shirika la habari la Anadolu la Uturuki limetangaza habari hiyo na kumnukuu msemaji wa jeshi la Libya, Kanali Mohammed Ganunu akitoa ufafanuzi kuhusu shambulio hilo na kusema, basi hilo limeshambuliwa karibu na eneo la Nasma, kusini mwa Tripoli.
Jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya, mapema jana asubuhi pia lilishambulia lori moja la mafuta la wanamgambo wa Khalifa Haftar na magari mawili ya kijeshi yaliyokuwa na silaha nzito kusini magharibi mwa Tripoli wakati magari hayo yalipokuwa yanaelekea katika maeneo yanayodhibitiwa na wanamgambo wa jenerali huyo muasi.
Jenerali Khalifa Haftar anaongoza wanamgambo wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya na anaungwa mkono na nchi za Saudi Arabia, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na baadhi ya nchi za Magharibi.
Tangu mwezi Aprili 2019 alianzisha vita vikubwa dhidi ya mji mkuu Tripoli kwa uungaji mkono wa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri na baadhi ya nchi za Magharibi. Lengo la kuanzisha vita hilo lilikuwa ni kuiteka Tripoli na kuivunja Serikali ya Mwafaka wa Kimataifa inayotambuliwa kimataifa. Hata hivyo ndoto za jenerali huyo muasi zimeshindwa kutimia kutokana na muqawama wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayoongozwa na Fayez al Sarraj.
Jumatatu wiki hii, Jenerali Khalifa Haftar alitangaza kuvunja makubaliano yaliyofikiwa tarehe 17 Disemba 2015 katika mji wa Skhirat Morocco, yaliyounda Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa hatua ambayo imelaaniwa kote duniani.