Guterres aelezea hofu yake kutokana kushiriki mamluki katika vita Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i60833-guterres_aelezea_hofu_yake_kutokana_kushiriki_mamluki_katika_vita_libya
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameelezea hofu kubwa aliyo nayo kutokana na kutumiwa mamluki katika vita vya Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 07, 2020 08:35 UTC
  • Guterres aelezea hofu yake kutokana kushiriki mamluki katika vita Libya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameelezea hofu kubwa aliyo nayo kutokana na kutumiwa mamluki katika vita vya Libya.

Shirika la habari la FARS limemnukuu Stéphane Dujarric, msemaji wa António Guterres akisema hayo mbele ya waandishi wa habari mjini New York Marekani alipozungumza nao kwa njia ya video na kuongeza kuwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ana wasiwasi mkubwa kutokana na kutumiwa mamluki katika vita vya Libya kwani nchi hiyo haihitajii mamluki bali inataka mshikamano na umoja wa kitaifa utakaorahisisha kutatuliwa kisiasa mgogoro wake.

Dujarric aidha amesema kuhusu kuteuliwa mjumbe mpya wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya kushika nafasi ya Ghassan Salamé kwamba mchakato wa kuainishwa mtu mwingine wa kushika nafasi hiyo bado unaendelea na kwa hivi sasa Bi Stephanie Williams ndiye anayekaimu nafasi hiyo hadi atakapotangazwa mjumbe maalumu mpya.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres

 

Mwezi Machi mwaka huu, Ghassan Salamé alitangaza kujiuzulu nafasi ya mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya baada ya kufanya kazi hiyo kwa takriban miaka mitatu. Alisema amelazimika kujiuzulu kutokana na kuumwa.

Salamé alilaumiwa na pande za Libya kutokana na msimamo wake wa kutangaza kuanza mazuhngumzo ya makundi ya Libya katika awamu tatu za kisiasa baada ya kikao cha amani cha Berlin, Ujerumani.

Wanamgambo wanaojiita "Jeshi la Taifa la Libya" wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar walianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa Libya, Tripoli, mwezi Aprili 2019 kwa uungaji mkono kamili wa Saudi Arabia, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu yaani Imarati kwa tamaa ya kuiangusha Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa, ndoto ambayo haijatimia hadi leo hii.