Wanamgambo wa Haftar waendelea kudondosha mabomu na kuua raia Libya
Wanamgambo wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya wanaoogozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar wameendelea kutekeleza mashambulizi mtawalia ya mabomu katika mji mkuu Tripoli, licha ya janga la corona na mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Katika shambulizi lake la jana Alkhamisi, wapiganaji hao wameua askari polisi wawili na raia mmoja karibu na balozi za Uturuki na Italia katikati mwa mji mkuu Tripoli.
Afisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Libya amesema vikosi hivyo vya Haftar vilidondosha mabomu manane hapo jana ambayo mbali na kuua, yameharibu pia majengo na miundomsingi ya eneo hilo, huku magari kadhaa pia yakiteketea kwa moto.
Aidha siku ya Jumatano, wapiganaji hao wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya wanaoogozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar walidondosha mabomu mengine Tripoli na kuua raia watano na kujeruhi makumi ya wengine.
Wanamgambo hao walisema katika taarifa ya Jumanne iliyopita kuwa, "asubuhi ya leo (Jumanne) kundi la waasi (Jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa) wamejaribu kufanya shambulizi la kioga dhidi ya uwanja wa ndege wa kijeshi wa Watya, yapata kilomita 140 kusini magharibi mwa mji mkuu Tripoli, chini ya himaya ya jeshi la anga la Uturuki, lakini tukajibu mapigo na kuua 40 miongoni mwao, mbali na kujeruhi na kuwatia mbaroni wengine wengi."
Wanamgambo wanaojiita "Jeshi la Taifa la Libya" wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar walianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa Libya, Tripoli, mwezi Aprili 2019 kwa uungaji mkono kamili wa Saudi Arabia, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu kwa tamaa ya kuiangusha Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa, ndoto ambayo haijatimia hadi leo hii.