Madai ya Uturuki kuhusu faida za uwepo wa majeshi yake nchini Libya
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlüt Çavuşoğlu amesema: “Uwepo wa wanajeshi wa Uturuki nchini Libya ni jambo litakalopelekea pande mbile hasimu nchini humo kuchukua hatua za kimsingi kuekelea katika usitishwaji vita.”
Akizungumza Jumapili, Çavuşoğlu alidai kuwa: “Wote wanakiri kuwa mlingano wa nguvu nchini Libya umebadilika baada ya kuingia Uturuki nchini humo na kama Uturuki haingeingia basi vita Libya vingefika mitaani.”
Madai Çavuşoğlu yamekuja baada ya matamshi ya waziri mwenzake wa ulinzi na wakuu wengine wa serikali ya Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki pamoja na pia weledi wa mambo wanaofungamana na chama tawala cha Uturuki cha AKP ambao halikadhalika wamedai kuwa uwepo wa majeshi ya Uturuki huko Libya umepelekea kuwepo mlingano wa nguvu nchini humo
Hata hivyo ukweli wa mambo ni kuwa, uwepo wa majeshi wa Uturuki nchini Libya umepelekea Serikali ya Muafaka wa Kitaifa (GNU) yenye makao yake Tripoli kupata nguvu zaidi na inaelekea kuwa serikali ya Uturuki inafuatilia malengo ya siri katika uingiliaji wake nchini Libya.
Uturuki inasema inaiunga mkono Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayazz Al Sarraj kwa sababu serikali hiyo inatambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa,
Wiki iliyopita, Waziri wa Ulinzi wa Uturuki Hulusi Akar aliashiria kubadilika mlingano wa nguvu nchini Libya na Kusema: “Baada ya kuanza ushirikiano wa Uturuki na askari wa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya, mlingano wa nguvu nchini Libya kwa kiasi kikubwa umekuwa ni kwa maslahi ya vikosi vinavyoungwa mkono na serikali ya Fayyaz Al-Sarraj.”
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya hivi karibuni ya Uturuki kwa wanasiasa wa nchi hiyo kuzungumza wa kujifakharisha kuhusu uwepo wa majeshi ya nchi hiyo katika nchi nyingine. Sababu ya matamshi hayo iko wazi kabisa. Serikali ya Uturuki inatumia uwezo wake wote kuhakikisha kuwa serikali ambayo inachukua madaraka kamili nchini Libya ni ile inayofungamana na harakati ya Kiislamu ya Ikwanul Muslimin. Halikadhalika Uturuki pia inafuatilia malengo ya kiuchumi nchini Libya. Katika upande wa pili, tawala zipingazo mabadiliko za Ghuba ya Uajemi, hasa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu ziko katika upande mkabala wa Uturuki na zinafanya juu chini kuhakikisha zinazuia serikali inayofungamana na Ikhwanul Muslimin kuchukua hatamu za uongozi kote Libya.
Kuhusiana na nukta hii, Profesa Ahmad Bakhshi, mhadhiri wa chuo kikuu na mtaalamu mwandamizi wa masuala ya Afrika hivi karibuni alisema: “Saudi Arabia na UAE pamoja na baadhi ya nchi za Ghuba ya Uajemi hazitaki kuona serikali inayofungamana na Ikhwanul Muslimin ikichukua madaraka nchini Libya. Mkabala wa hilo, serikali ya Uturuki ambayo inaunga mkono Harakati ya Ikwanul Muslimin nayo inalenga kuhuisha satwa wa utawala wa Kiuthmaniya. Hakuna shaka kuwa, kuchukua madaraka harakati hiyo ya Ikwanul Muslimin ni kengele ya hatari wa tawala wa Kiarabu kama vile Saudi Arabia na Imarati.”

Pamoja na ukweli huo, hakuna shaka kuwa, uwepo wa Uturuki nchini Libya kutazidisha hitilafu za Ankara na baadhi ya nchi za Kiarabu na Ulaya. Kwa mfano hivi karibuni nchi tatu za Ulaya na nchi mbili za Kiarabu zilitoa taarifa kali na kulaani sera za kijeshi za Uturuki nchini Libya, Bahari ya Mediteranea, Bahari ya Aegean na hata Syria. Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki nayo ilitoa taarifa kujibu tamko la nchi hizo tano dhidi ya serikali ya Ankara na kusema: “Mhimili wa shari umeundwa dhidi ya Uturuki.”
Kuhusiana na nukta hii, tunapaswa kusema kuwa Uturuki na nchi za Kiarabu za UAE, Saudi Arabia na Misri sambamba na kuanza mashindano ya kimataifa ya silha na kila moja ya nchi hizo inajaribu kuwa yenye nguvu zaidi za kijeshi.
Mbali na ukweli huu, hakuna shaka kuwa uwepo wa kijeshi wa Uturuki nchini Libya kutashadidisha hali ya kutoaminiana serikali za kieneo. Kwa hivyo matatizo baina ya serikali za eneo yataendelea kuwa mabaya zaidi siku za usoni. Hakuna shaka kuwa, hali hii itahatarisha serikali na mataifa ya maeneo.