Kanisa Katoliki Burundi lasema uchaguzi wa rais uligubikwa na kasoro nyingi
Kanisa Katoliki nchini Burundi limetilia shaka matokeo ya uchaguzi wa rais wa Mei 20 uliompa ushindi mgombea wa chama tawala CNDD-FDD.
Baraza la Maaskofu wa Katoliki Burundi limesema waangalizi wake waliokuwepo katika vituo vya kupiga kura nchini humo walishuhudia masanduku ya kura yakifunguliwa, mbali na maafisa wa serikali kuwadhalilisha na kuwatisha wapiga kura.
Baraza hilo limesema uchaguzi huo ulizungukwa na mizengwe mingi, ambapo baadhi ya watu walipiga kura kwa kutumia majina ya watu waliofariki dunia na wakimbizi.
Mkuu wa Baraza la Maaskofu Burundi Askofu Joachim Ntahondereye amesema zoezi la kuhesabu kura kwenye uchaguzi wa urais nchini humo lilifanyika kwa usiri mkubwa.
Tume ya Uchaguzi ya Burundi (CENI) siku ya Jumapili ilimtangaza mgombea wa chama tawala CNDD-FDD, Evariste Ndayishimie mshindi wa uchaguzi wa rais kwa kuzuoa asilimia 68.72 ya kura.
Hata hivyo, Agathon Rwasa, mgombea wa chama kikuu cha upinzani cha CNL ambaye aliibuka wa pili kwa asilimia 24.19 amelalamikia matokeo hayo na kusema kumefanyika udanganyifu mkubwa. Chama chake kilitarajiwa kufikia jana Jumatano kiwe kimewasilisha faili la kupinga matokeo hayo katika Mahakama ya Katiba. Mahakama hiyo ndiyo inayopaswa kuidhinisha ushindi wa uchaguzi wa rais kufikia Juni 4.
Rais anayeondoka, Pierre Nkurunziza ambaye yuko madarakani tokea mwaka 2005, amempongeza jenerali huyo zamani wa kijeshi kwa kushinda kiti cha rais.