Rais Nkurunziza wa Burundi ameaga dunia kufuatia 'mshtuko wa moyo'
Rais Nkurunziza wa Burundi ameaga dunia kufuatia 'mshtuko wa moyo'
-
Pierre Nkurunziza
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza ameaga kutokana na kile ambacho kimetajwa ni mshtuko wa moyo.
Kwa mujibu wa ujumbe Twitter wa serikali ya Burundi, Rais Pierre Nkurunziza aliyekuwa na umri wa miaka 55 amefariki kwa mshtuko wa moyo leo Juni 8, 2020 katika Hospitali ya Cinquantenaire katika mji Karusi
Serikali ya Burundi imetangaza siku saba za maombolezo na imetuma salamu za ramirambi kwa familia.
Aidha, serikali inasema kuwa alilazwa hospitalini Jumamosi iliyopita na akapata mshtuko wa moyo mapema hii leo licha ya juhudi za kumuokoa ambazo hazikufua dafu.
Rais Pierre Nkurunziza alikuwa ameratibiwa kumkabithi mrithi wake madaraka jenerali Evariste Ndayishimiye.
Nkurunziza aliingia madarakani Burundi tangu mwaka 2005 na mwaka 2015 alichaguliwa tena katika uchaguzi uliokuwa na utata kufuatia mabadiliko ya katiba yaliyomuwezesha kutawala kwa muhula wa tatu.
Katika uchaguzi uliofanyika Mei mwaka huu, Nkurunziza hakugombea na mgombea wa chama tawala, Evariste Ndayishimiye ndiye aliyeibuka mshindi.
Evariste atachukua nafasi ya Rais Pierre Nkurunziza ambaye ameliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki kwa miaka 15.
Ndayishimiye ni mwanasiasa wa karibu wa Nkurunziza na amekuwa Katibu Mkuu wa Chama tawala cha CNDD-FDD tangu mwaka 2016.
Alizaliwa mwaka wa 1968 katika mkoa wa Gitega, eneo la kati mwa taifa hilo.
Nkurunziza ameaga dunia siku 10 tu baada ya mke wake, Denise Bucumi Nkurunziza kupelekwa kwa ndege mjini Nairobi, Kenya kupata matibabu baada ya kuambukizwa COVID-19.