Mahakama ya Katiba yaamua Ndayishimiye aapishwe mapema kuwa rais wa Burundi
Mahakama ya Kikatiba ya Burundi imeamua kuwa Evariste Ndayishimiye aliyeshinda uchaguzi mkuu wa hivi karibuni nchini Burundi aapishwe mapema kuwa rais wa nchi hiyo kufuatia kifo cha ghafla cha Rais Pierre Nkurunziza.
Uamuzi wa kuikabidhidi mahakama hiyo jukumu hilo ulifikiwa katika mkutano wa Baraza la Mawaziri la nchi hiyo Alkhamisi, baada ya taifa hilo kushuhudia ombwe la uongozi kufuatia kifo cha Nkurunziza.
Rais Nkurunziza aliaga dunia Jumatatu iliyopita kutokana na kile kilitajwa na serikali ya Bujumbura kuwa ni mshtuko wa moyo.
Kwa mujibu wa Katiba ya Burundi, Spika wa Bunge la nchi hiyo, Pascal Nyabenda ndiye aliyepaswa kushika madaraka ya nchi hadi wakati wa kuapishwa rasmi rais mteule, Evariste Ndayishimiye mwezi Agosti mwaka huu.
Hata hivyo taarifa ya serikali ya Bujumbura ilisema kuwa, Mahakama ya Kikatiba ya nchi hiyo ndiyo iliyopewa jukumu la kutoa muongoza na uamuzi a mwisho juu ya suala hilo.
Katika uchaguzi uliofanyika Mei mwaka huu, Nkurunziza hakugombea na mgombea wa chama tawala CNDD-FDD, Evariste Ndayishimiye ndiye aliyeibuka mshindi.
Kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama hiyo sasa Jenerali mstaafu Evariste Ndayishimiye amechukua nafasi ya Pierre Nkurunziza ambaye ameliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki kwa miaka 15.