Waliouawa katika ghasia Ethiopia wafika 239
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62079-waliouawa_katika_ghasia_ethiopia_wafika_239
Mauaji ya watu hao yamejiri katika ghasia ambazo ziliiibuka Ethiopia wiki iliyopita kufuatia mauaji ya mwanamuziki na mwanaharakati maarufu Haacaaluu Hundeessaa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 08, 2020 11:34 UTC
  • Waliouawa katika ghasia Ethiopia wafika 239

Mauaji ya watu hao yamejiri katika ghasia ambazo ziliiibuka Ethiopia wiki iliyopita kufuatia mauaji ya mwanamuziki na mwanaharakati maarufu Haacaaluu Hundeessaa.

Mwanaharakati huyo, kutoka kabila la Oromo, alipigwa risasi na kuuawa na watu wasiojulikana Jumatatu usiku katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa. Mauaji hayo yameibua uhasama wa kikabila katika nchi hiyo ambayo iko katika mchakato wa kuelekea katika demokrasia kamili.

Kaimu Kamishna wa Polisi katika eneo la Oromia, Mustafa Kedir alitoa taarifa Jumatano na kusema raia 215 na maafisa tisa wa usalama pamoja na wanamgamo 15 wameuawa katika ghasia ambazo zimeibuka eneo hilo. Watu wengine 10 wanaripotiwa kuuawa katika ghasia mjini Addis Ababa. Awali idadi ya waliofariki katika ghasia hizo ilikuwa imeripotiwa kuwa ni 166. Aidha Mustafa Kedir amesema zaidi ya watu 3,500 wametia mbaroni kwa kuhusika na ghasia hizo.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema ghasia ambazo zilishuhudiwa kwa muda wa siku tatu nchini humo zilikuwa ni njama ya kuibua vita vya ndani na sasa njama hiyo imezimwa.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Hundeessaa, 34, ambaye ni kutoka kabila la Oromo alikuwa mashuhuri kwa nyimbo zake za kimapinduzi na kutetea haki.

Wafuasi wake wanasema aliuawa kutokana na nyimbo zake ambazo zilikuwa zinawahimiza watu wa kabila la Oromo waamke kutetea haki zao na wapambane na ukandamizaji. Ingawa kabila la Oromo ndilo kubwa zaidi nchini Ethiopia lakini kwa muda mrefu Waoromo wamekuwa wakilalamika kuwa  wanabaguliwa na kutengwa. Baba yake Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ni kutoka kabila la Oromo na mama yake ni kutoka kabila la Amhara.