Watu 4 wauawa katika maandamano ya ghasia Kongo DR
Watu wanne wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika maandamano ya kupinga uteuzi wa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Tume ya Pamoja ya Kutetea Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (UNJHRO) imethibitisha habari za mauaji hayo na kulaani kitendo cha polisi ya DRC cha kutumia nguvu kupita kiasi kuzima maandamano ya wananchi.
Kwa akali waandamanaji watatu wameuawa katika maandamano hayo mbali na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Katika maandamano hayo ya jana Alkhamisi, askari polisi walitumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuzima maandamano hayo ya ghasia baina ya wafuasi wa Rais Felix Tshisekedi wa nchi hiyo na makundi ya kiraia yanayopinga uteuzi wa mwenyekiti mpya wa Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (CENI).
Kadhalika Tume ya Pamoja ya Kutetea Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imelaani mauaji ya askari polisi mmoja katika maandamano hayo ya ghasia yaliyoshuhudiwa katika mji mkuu KInshasa, Lubumbashi, Goma na miji mingine midogo ya nchi hiyo.

Kambi ya upinzani na makundi ya kiraia ya nchini humo yanapinga uteuzi wa Ronsard Malonda kuwa Rais wa CENI, wakidai kuwa ni mpambe wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Joseph Kabila, ambaye wanahisi angali na mamlaka na anaiendesha nchi nyuma ya pazia.
Uteuzi wa Malonda ulipasishwa wiki iliyopita na Bunge la nchi hiyo ambalo aghalabu ya wanachama wake ni wafuasi wa chama cha Kabila, na hivi sasa anasubiri saini ya rais ili akabidhiwe rasmi ofisi.