Tanzania yatangaza tarehe ya uchaguzi mkuu mwaka huu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62337-tanzania_yatangaza_tarehe_ya_uchaguzi_mkuu_mwaka_huu
Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC) imetangaza tarehe rasmi ya Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki pamoja na ratiba rasmi ya kuanza kwa mikutano ya kampeni.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 22, 2020 02:31 UTC
  • Tanzania yatangaza tarehe ya uchaguzi mkuu mwaka huu

Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC) imetangaza tarehe rasmi ya Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki pamoja na ratiba rasmi ya kuanza kwa mikutano ya kampeni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Jumanne na Tume ya Uchaguzi ya Tanzania ni kwamba, uchaguzi mkuu utafanyika Oktoba mwaka huu 2020. 

Uchaguzi huo ni ule wa Urais, na Ubunge na Udiwani Tanzania Bara. Kwa kujibu wa tume hiyo, kampeni za uchaguzi huo zitaanza rasmi August 26 mpaka Oktoba 27 mwaka huu 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Jumanne, Mwenyekiti wa NEC, Semistocles Kaijage amesema, "uchaguzi mkuu utafanyika Jumatano ya Oktoba 28 mwaka huu, huku kampeni zikitarajiwa kuanza August 26 hadi Oktoba 27, 2020. Aidha uteuzi wa Wagombea wa kiti cha Urais, Makamu wa Rais, Ubunge na Udiwani utafanyika August 25, mwaka huu 2020."

Rais Magufuli (kushoto) na Tundu Lissu, kinara wa upinzania Tanzania

Hii ni katika hali ambayo, licha ya kupongezwa kwa hatua mbalimbali za maendeleo zilizochukuliwa na serikali yake, zikiwemo za kustawisha miundomsingi ya kiuchumi na kupambana na ufisadi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli amekuwa akikosolewa kwa madai kuwa anaminya na kukandamiza demokrasia sambamba na kuendesha kampeni ya kuua vyama vya upinzani katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Wanasiasa wa upinzani wanadai kuwa serikali ya sasa ya Rais Magufuli imeweka mazingira magumu ya kufanya mikutano ya kisiasa na hivyo kukandamiza demokrasia.