Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, anazikwa leo
Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin William Mkapa anazikwa leo katika kijiji alichozaliwa cha Lupaso katika Wilaya ya Masasi, mkoa wa Mtwara Kusini mwa nchi hiyo.
Mkapa alifariki usiku wa kuamkia Ijumaa kutokana na mshtuko wa moyo, familia yake ilieleza.
Rais John Magufuli amewaongoza waombolezaji hao wakiwemo wawakilishi wa maitafa ya kigeni nchini humo.
Tayari mwili wa Mkapa umewasili katika kijiji alichozaliwa kwa mazishi.
Mkapa aliyeongoza Tanzania kati ya mwaka 1995-2005 alifariki dunia kutokana na mshtuko wa moyo.
Baada ya kumaliza utawala wake, Mkapa alianzisha taasisi binafsi ambayo iliongoza mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi nchini humo.
Rais huyo atakumbukwa kuwa kiongozi ambaye ni mwanadiplomasia na kushiriki katika shughuli nyingi za Umoja wa Mataifa pamoja na kutatua migogoro katika mataifa ya Afrika.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Mohamed Mahmat Faki, amemuomboleza Mkapa kwa kuandika ujumbe ufuatao katika akaunti yake ya Twitter; "Afrika imepoteza mpatanishi".
Mkapa, akiwa na Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa (UN), hayati Koffi Annan na Graca Machel walikuwa wapatanishi wa mgogoro wa kisiasa wa Kenya uliotokana na Uchaguzi Mkuu wa Desemba mwaka 2007. Upatanishi huo ulizuia umwagikaji zaidi wa damu katika nchi hiyo. Baada ya kifo cha Mkapa, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alitangaza siku tatu za maombolezo rasmi ya kitaifa.