Kuongezeka opereseheni za jeshi la Somalia dhidi ya ash Shabab
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6253-kuongezeka_opereseheni_za_jeshi_la_somalia_dhidi_ya_ash_shabab
Kamanda mmoja wa jeshi la Somalia amesema kuwa, jeshi la nchi hiyo limeshadidisha operesheni zake dhidi ya kundi la ash Shabab kusini mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 02, 2016 12:27 UTC
  • Kuongezeka opereseheni za jeshi la Somalia dhidi ya ash Shabab

Kamanda mmoja wa jeshi la Somalia amesema kuwa, jeshi la nchi hiyo limeshadidisha operesheni zake dhidi ya kundi la ash Shabab kusini mwa nchi hiyo.

Shirika la habari la Xinhua limemnukuu Abdullah Yusuf kamanda mwandamizi wa jeshi la Somalia katika eneo la Shabeellah Hoose la kusini mwa Somalia akisema kuwa, jeshi la nchi hiyo kwa kushirikiana na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika wameanzisha duru mpya operesheni za kijasusi na kijeshi katika eneo hilo.

Inafaa kusema kuwa, eneo la Shabeellah Hoose la kusini mwa Somalia bado ni ngome kuu ya kundi la ash Shabab.

Abdullah Yusuf ameongeza kuwa, operesheni za jeshi la Somalia dhidi ya kundi la ash Shabab zitaendelea hadi litakapotokomezwa kabisa kundi hilo katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Ikumbukwe kuwa, jana kulitokea mripuko wa bomu katika soko moja la mifugo katika eneo hilo na kupelekea wanajeshi wasiopungua wawili wa serikali kuuawa na watu wengine wanane kujeruhiwa.

Mwaka 2006 kundi la ash Shabab ambalo limetangaza uungaji mkono wake kwa mtandao wa al Qaida, liliteka maeneo mengi ya Somalia kabla ya kuzidiwa nguvu na kurejeshwa nyuma na vikosi vya Umoja wa Afrika vikishirikiana na serikali ya Somalia.