Mafuriko yaua makumi ya watu na wengine wapoteza makazi Abuja, Nigeria
-
Abuja, Nigeria
Mafuriko makubwa yaliyotokea katika kitongoji kimoja cha mji mkuu wa Nigeria, Abuja na mji mwingine wa nchi hiyo, yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 30.
Maafisa wa serikali ya Nigeria wametangaza kuwa, mafuriko hayo ambayo yametokea katika kitongoji cha Gwagwalada mjini Abuja na katika mji wa Suleja pia yameharibu mamia ya nyumba za wakazi wa maeneo hayo.
Ripoti zinasema kuwa mamia ya watu wamelazimika kukimbia makazi na nyumba zao kutokana na mafuriko hayo ambayo maafisa wa serikali wanasema yamesababisha hasara kubwa.
Timu za ukoaji za serikali ya Nigeria zilikuwa zinaendelea kutafuta manusura na kutoa misaada kwa waathirika wa mafuriko hayo.
Mvua kubwa iliyonyesha katika eneo la Dei-Dei, Gwagwalada, yapata wiki moja iliyopita pia ilisababisha vifo vya watu wasiopungua 6 na hasara kubwa ya mali.

Mji mkuu wa Nigeria, Abuja, umekuwa ukikumbwa na mafuriko ya mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni ambayo yamesababisha vifo vya watu na hasara kubwa ya mali.