Sudan iko tayari kushirikiana na ICC kuhusu jinai za kivita Darfur
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i62975
Serikali ya Sudan imesema iko tayari kushirikiana na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ili kuhakikisha kuwa washukiwa wa jinai za kivita katika eneo la Darfur wanafikishwa mbele ya korti hiyo yenye makao yake mjini Hague nchini Uholanzi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 23, 2020 07:56 UTC
  • Abdalla Hamdok
    Abdalla Hamdok

Serikali ya Sudan imesema iko tayari kushirikiana na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ili kuhakikisha kuwa washukiwa wa jinai za kivita katika eneo la Darfur wanafikishwa mbele ya korti hiyo yenye makao yake mjini Hague nchini Uholanzi.

Hayo yalisemwa jana Jumamosi na Waziri Mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok, hii ikiwa ni mara ya kwanza kutangaza hadharani msimamo huo wa serikali yake, ingawaje mwezi Februari mwaka huu, serikali hiyo ilifikia makubaliano na makundi mbalimbali ya waasi na wapinzani katika eneo la Darfur, magharibi mwa Sudan juu ya kukabidhiwa washukiwa wote watano wa Kisudani wanaohusishwa na jinai hizo za kivita akiwemo aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Omar Hassan al-Bashir.

Al-Bashir ambaye alipinduliwa na jeshi mwezi Aprili mwaka jana kufuatia maandamano ya miezi kadhaa ya wananchi dhidi ya utawala wake, anasakwa na mahakama ya ICC kwa tuhuma za mauaji ya kimbari, jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu huko Darfur magharibi mwa Sudan. 

Hamdok amesisitiza kuwa, "nakariri tena kuwa, serikali (ya Sudan) iko tayari kushirikiana na ICC ili kuhakikisha kuwa mahakama hiyo inawahukumu washukiwa wa jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu."

Mafuvu yanayoashiria ukubwa wa jinai za kivita eneo la Darfur

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai mwaka 2008 na 2009 ilitoa waranti wa kukamatwa Omar al-Bashir na watu wengine 51 kwa tuhuma za kutenda jinai za kivita na maangamizi ya kizazi katika jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan. 

Eneo la Darfur mwaka 2003 lilikumbwa na mapigano ya umwagaji damu kati ya serikali ya wakati huo ya Sudan chini ya uongozi wa Rais al-Bashir, na wapinzani wa serikali. Karibu wakazi 300,000 wa jimbo hilo waliuawa katika mapigano hayo.