Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania awasili Pemba kukabiliana na 'wachochezi'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63210-mkuu_wa_jeshi_la_polisi_tanzania_awasili_pemba_kukabiliana_na_'wachochezi'
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania Simon Sirro amewasili kisiwani Pemba, Zanzibar kwa ajili ya kile kilichotajwa kuwa kufanya vikao na vyama vya siasa na viongozi wa dini kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi ujao.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 04, 2020 07:03 UTC
  • IGP Sirro
    IGP Sirro

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania Simon Sirro amewasili kisiwani Pemba, Zanzibar kwa ajili ya kile kilichotajwa kuwa kufanya vikao na vyama vya siasa na viongozi wa dini kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi ujao.

 IGP Sirro amesema lengo kufanya mikutano hiyo ni kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu ujao unafanyika kwa amani na salama. 

Vyombo vya habari vimemnukuu Sirro akisema kuwa, “Ndoto yetu sisi Polisi tutende haki ili tuwe na uchaguzi wa amani. Pemba nimekuja kuongea na Kamati za Ulinzi na Usalama, Viongozi wa dini na Viongozi wa Siasa tukubaliane maana wote ni sehemu ya Uchaguzi, nitatoa elimu na kuna wengine nitawapa elimu lakini hawatoifuata.”

Kadhalika Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania amesema, “Nitawagonga, wanasema wapo tayari, nitawapa elimu hawaendi pazuri.”

Haya yanajiri baada ya kuenea katika mitandao ya kijamii kanda ya video inayoonyesha mkusanyiko mkubwa wa watu ukumbini kisiwani Pemba, huku mmoja akiihutubia hadhira na kuwataka wawe tayari kwa ajili ya mapambano ya kushinikiza kurejeshwa wagombea wao wa ubunge na udiwani kwenye kinyang'ayiro cha uchaguzi. Tume ya Uchaguzi nchini humo imefuta baadhi ya majina ya wagombea kwa kile ilichokitaja kuwa, hawajatimiza vigezo na masharti ya kuwania viti hivyo.

Uchaguzi mkuu nchini Tanzania umepangwa kufanyika tarehe 28 ya mwezi ujao wa Oktoba

Haya yanajiri siku chache baada ya Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) kutangaza kuwa, mamlaka nchini Tanzania imeongeza hatua za ukandamizaji dhidi ya vyama vya upinzani na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu hapo mwezi ujao. 

Uchaguzi mkuu nchini Tanzania umepangwa kufanyika tarehe 28 ya mwezi ujao wa Oktoba na hivi sasa tayari kampeni za uchaguzi huo zinaendelea licha ya manung'uniko ya kambi ya upinzani kuhusiana na masuala mbalimbali kama kutokuweko tume huru ya uchaguzi, kutofanyika mabadiliko ya katiba na hata vyombo vya usalama kuonekana vinakipendelea chama tawala CCM.