Mkoa wa Tigrey nchini Ethiopia kuendesha uchaguzi; umekaidi agizo la serikali
Mkoa wa Tigrey wa kaskazini mwa Ethiopia umepanga kuendesha uchaguzi Jumatano ijayo ikiwa ni kukaidi agizo la serikali ya shirikisho ya nchi hiyo.
Hatua hiyo imetajwa na weledi wa mambo kuwa ni changamoto mbele ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed.
Waziri Mkuu wa Ethiopia amesimamia mageuzi makubwa ya kidemokrasia tangu ashike hatamu za uongozi miaka miwili iliyopita katika nchi hiyo ya pili barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya watu.
Itakumbukwa kuwa, serikali ya shirikisho ya Ethiopia na vyama vikuu vya upinzani vilikubaliana kuakhirisha uchaguzi wa taifa na wa mikoa uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi Agosti ili kudhibiti kwanza maambukizi ya corona nchini humo. Lakini mkoa wa Tigray ambao viongozi wake wanadhibiti serikali ya sasa wametangaza kuwa mkoa wao huo utaendesha uchaguzi huo na hautosikiliza agizo la serikali kuu. Getachew Reda, Waziri wa zamani wa habari wa serikali ya shirikisho ya Ethiopia ambaye sasa ni msemaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray amesema kuwa, wanafahamu kwamba kuna vitisho vya wazi kutoka kwa Abiy Ahmed kwamba jeshi litaingilia kati dhidi yetu na pia serikali itatukatia misaada ya fedha lakini licha ya kuweko vitisho hivyo wao wataitisha uchaguzi kama walivyopanga.
Kabila la Watigraya ni jamii pekee ya walio wachache katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika iliyo na watu wapatao milioni 110 lakini ni kabila ambalo limekuwa likishikilia madaraka tangu ya nchi mwaka 1991 wakati Harakati ya Kidemokrasia ya Kimapinduzi ya Watu wa Ethiopia ilipomuondoa madarakani dikteta mwanajeshi mwenye mielekeo ya kimaksi, Mengistu Haile Mariam.