Raia 3 wa Ethiopia wafia katika kambi ya kuzuilia wahajiri Saudia
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetangaza habari ya kupoteza maisha wahamiaji watatu wa Kiethiopia ambao walikuwa wanashikiliwa katika mazingira yasiyo ya kibinadamu nchini Saudi Arabia.
Ripoti iliyotolewa leo Ijumaa na shirika hilo imesema maelfu ya wahajiri hao wa Kiethiopia wanapitia kipindi kigumu katika vituo vya kuwazuilia nchini Saudia, na hali imekuwa mbaya zaidi katika kipindi hiki cha janga la corona.
Mtafiti wa Amnesty International, Marie Forestier amesema katika taarifa kuwa, "maelfu ya raia wa Ethiopia walielekea Saudi Arabia kwa ajili ya kutafuta maisha mazuri, lakini badala yake wamekumbana na hali ngumu na isiyo ya kibinadamu."
Ameitaka serikali ya Riyadh iwaachie huru wahajiri inayowazuilia kinyume cha sheria, na vile vile iboreshe hali ya kambi inazotumia kuwazuilia wahamiaji hao.

Mwezi uliopita, serikali ya Ethiopia ilitangaza kuwa itawarejesha nyumbani wahajiri karibu 2,000 kutoka Saudi Arabia katika wiki zijazo, kutokana na wasiwasi mkubwa wa jamii ya kimataifa juu ya hali mbaya inayoshuhudiwa katika kambi za wahamiaji nchini humo.
Kabla ya hapo pia, Human Rights Watch iliripoti kuwa makumi ya wahajiri wa Kiethiopia waliokimbia vita kaskazini mwa Yemen wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa mpakani wa Saudi Arabia.