ICC kuendelea kumzuilia kinara wa washukiwa wa jinai za kivita Darfur
Majaji wa Kitengo cha Rufaa cha Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) wamepasisha uamuzi wa kuendelea kumshikilia kinara wa kundi la wanamgambo wanaoshukiwa kuhusika na jinai za kivita katika eneo la Darfur nchini Sudan mwaka 2003.
Katika uamuzi wa jana Alkhamisi, majaji hao wamekataa ombi la mshukiwa huyo Ali Mohammed Ali Abdul Rahman Ali, ambaye anafahamika pia kama Ali Kushayb la kutaka aachiwe huru huku kesi yake ikiendelea kusikilizwa katika mahakama hiyo ya mjini Hague nchini Uholanzi.
Kushayb ambaye anaandamwa na mashitaka 50 ya jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu katika vita vya Darfur alipelekwa Hague mwezi Juni mwaka huu, ikiwa imepita miaka 13 tangu majaji wa ICC watoe waranti dhidi yake.
Kikao cha kuamua iwapo kuna ushahidi wenye mashiko wa kumfungulia kesi kamili mshukiwa huyo au la kinatazamiwa kufanyika Disemba 7 mwaka huu.
Mwaka 2008 na 2009, ICC ilitoa waranti wa kukamatwa na watu zaidi ya 50 kwa tuhuma za kutenda jinai za kivita na maangamizi ya kizazi katika jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan, akiwemo aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Omar Hassan al-Bashir.
Eneo la Darfur mwaka 2003 lilikumbwa na mapigano ya umwagaji damu kati ya serikali ya wakati huo ya Sudan chini ya uongozi wa Rais al-Bashir, na wapinzani wa serikali. Karibu wakazi 300,000 wa jimbo hilo waliuawa katika mapigano hayo, mbali na wengine zaidi ya milioni 2.7 wakifurushwa kutoka kwenye nyumba zao.