Al-Shabaab inakusanya ushuru mkubwa zaidi ya serikali ya Somalia
(last modified Wed, 28 Oct 2020 04:38:00 GMT )
Oct 28, 2020 04:38 UTC
  • Al-Shabaab inakusanya ushuru mkubwa zaidi ya serikali ya Somalia

Ripoti mpya imefichua kuwa, kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab linakusanya kodi na ushuru mkubwa hata zaidi ya ule unaokusanywa na serikali ya Somalia.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Taasisi ya Hiraal, wanachama wa kundi hilo wanatumia vitisho, nguvu na mabavu kukusanya eti ushuru na zaka kutoka kwa wananchi wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Kwa mujibu wa ripoti ya taasisi hiyo, genge hilo la ukufurishaji kwa mwezi linakusanya kodi ya zaidi ya dola milioni 15, huku zaidi ya asilimia 50 ya fedha hizo zikikusanywa katika mji mkuu, Mogadishu. Hii ni katika hali ambayo, mwaka jana, serikali ya federali ya Somali ilikusanya dola milioni 230 kama ushuru wa ndani ya nchi.

Uchunguzi uliofanywa na taasisi hiyo umebainisha kuwa, karibu mashirika yote makubwa ya Somalia hususan ya kibiashara yanalipa kundi hilo fedha kwa njia mbili, ushuru unaokusanywa kila mwezi, na 'Zaka ya Mali' ya kila mwaka. 

Baadhi ya wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab la Somalia

Zakatul Maal ni asilimia 2.5 ya faida au pato ambayo hutolewa kwa watu makhsusi kila mwaka na watu waliotimiza vigezo vilivyowekwa na Uislamu; lakini genge hilo linakusanya fedha hizo kwa kutumia mabavu na vitisho.

Mwaka jana, wazee wanane katika eneo la Galmudug nchini Somalia waliuawa kwa kukatwa vichwa na kundi moja la wanamgambo lenye mfungamano na al-Shabaab, eti kwa kukataa kulipa kodi na 'zaka'.

Kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, kundi la kigaidi la al-Shabaab linaendesha uasi unaolenga kuvitimua vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika vilivyoko nchini Somalia AMISOM, kuiangusha serikali ya nchi hiyo na kuunda kile linachodai kuwa ni 'utawala wa Kiislamu' katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Tags