Ethiopia yasema uasi Tigray unachochewa na madola ya kigeni
Serikali ya Ethiopia imesema imeamua kutumia nguvu za kijeshi katika eneo la Tigray baada ya kupokea taarifa za kijasusi kuwa serikali yenye mamlaka ya ndani ya eneo hilo inapokea misaada ya kigeni kuchukua hatua dhidi ya serikali kuu iliyoko Addis Ababa.
Duru za ngazi za juu katika serikali ya Ethiopia zimelidokezea gazeti la Daily Nation la nchini Kenya kuwa, Waziri Mkuu Abiy Ahmed atachukua hatua kali baada ya kupokea habari kuwa eneo la Tigray limepokea msaada wa kijeshi ambao umepelekea kundi la TPLF kupata uwezo wa kushambulia kambi ya jeshi la serikali.
Hakuna taarifa kuhusu idadi ya waliouawa au kujeruhiwa katika hujuma hiyo ya Jumatano asubuhi. Bunge la Ethiopia limeidhinisha hali ya hatari ya muda wa miezi sita katika eneo la Tigray.
Imedokezwa kuwa uasi wa eneo la Tigray unahusiana na mzozo wa Bwawa la Grand Renaissance linalojengwa na Ethiopia. Ujenzi wa bwaba hilo ambalo limegharimu dola bilioni 4.5 unapingwa na Sudan na Misri ambazo zinasema bwawa hilo likijazwa kutakuwa na uhaba wa maji katika nchi hizo mbili.
Siku chache zilizopita Rais Donald Trump wa Marekani alisema Misri inaweza kutumia nguvu za kijeshi kusitisha ujenzi wa bwawa hilo la Ethiopia, matamshi ambayo yalilamikiwa vikali na wakuu wa Ethiopia.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres amesema ana wasiwasi mkubwa kuhusu mapigano yanayoendelea katika jimbo hilo la kaskazini mwa Ethiopia la Tigray, ambalo wanajeshi wa serikali kuu wamekuwa wakipambana na kundi lenye nguvu la kikabila ambalo liliuongoza muungano tawala kwa miongo mingi. Guterres amesema utulivu wa Ethiopia ni muhimu kwa eneo zima la Pembe ya Afrika. Ametoa wito wa kusitishwa mapigano na kutafutwa suluhisho la mgogoro huo kwa njia ya amani.