Bunge la Ethiopia laafiki kuundwa serikali katika eneo la Tigray
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i64485-bunge_la_ethiopia_laafiki_kuundwa_serikali_katika_eneo_la_tigray
Baada ya mapigano makali ya hivi karibuni baina ya vikosi vya serikali ya Ethiopia na vile vya Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray (The Tigray People's Liberation Front (TPLF), hatimaye Bunge la nchi hiyo limeafiki kuundwa serikali ya muda katika eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 07, 2020 07:24 UTC
  • Bunge la Ethiopia laafiki kuundwa serikali katika eneo la Tigray

Baada ya mapigano makali ya hivi karibuni baina ya vikosi vya serikali ya Ethiopia na vile vya Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray (The Tigray People's Liberation Front (TPLF), hatimaye Bunge la nchi hiyo limeafiki kuundwa serikali ya muda katika eneo hilo.

Uamuzi huo wa Bunge la Ethiopia umechukuliwa baada ya kushadidi hitilafu na mzozo baina ya serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed na viongozi wa eneo la Tigray.

Mwezi Septemba mwaka huu, wakazi wa mkoa wa Tigray wa kaskazini mwa Ethiopia walishiriki katika uchaguzi wa Bunge hatua ambayo ilikuwa kinyume kabisa na agizo la serikali ya shirikisho ya nchi hiyo.

Serikali ya Ethiopia na vyama vikuu vya upinzani vilikubaliana kuakhirisha uchaguzi wa taifa na wa mikoa uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi Agosti ili kudhibiti kwanza maambukizi ya corona nchini humo. 

Wapiganaji wa harakati ya Tigray ya TPLF 

 

Lakini mkoa wa Tigray ambao viongozi wake wanadhibiti serikali ya sasa walikataa kuakhirisha uchaguzi huo.

Baada ya uchaguzi huo, hitilafu baina ya serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed zilishadidi na kupelekea kutangazwa hali ya hatari katika eneo hilo na hivi karibuni kuanzishwa operesheni kali ya kijeshi dhidi ya Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray.

Kabila la Watigraya ni jamii pekee ya walio wachache nchini Ethiopia lakini ni kabila ambalo limekuwa likishikilia madaraka tangu mwaka 1991 wakati Harakati ya Kidemokrasia ya Kimapinduzi ya Watu wa Ethiopia ilipomuondoa madarakani dikteta mwanajeshi mwenye mielekeo ya kimaksi, Mengistu Haile Mariam.