Wakazi wa Amhara nchini Ethiopia waunga mkono oparesheni ya jeshi huko Tigray
Wakazi wa jimbo la Amhara kaskazini mwa Ethiopia linalopakana na eneo la Tigray wamesema kuwa wapo tayari kuliunga mkono jeshi la ulinzi ya nchi hiyo katika mzozo na harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF).
Wakazi wa eneo hilo wamenukuliwa wakisema kuwa makundi ya kikaumu ya eneo la kaskazini hayawezi kutenganishwa si kidini au kikabila. Wamesema jamii zao zina umoja na zimekuwa zikiishi pamoja kwa muda mrefu.
Jeshi la Taifa la Ethiopia linatumia kambi za kijeshi zilizoko katika jimbo la Amhara kuyashambulia maeneo mbambalimbali Tigray. Jana Jumapili Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alimfuta kazi Mkuu wa Jeshi na kusema kuwa nchi hiyo inajiandaa kwa ajili ya kampeni ya oparesheni ya muda mrefu huko Tigray. Waziri Mkuu wa Ethiopia pia amemteua Temesgen Tiruneh ambaye alikuwa mkuu wa Jimbo la Amhara kuwa Mkuu wa Idara ya Ujasusi ya nchi hiyo.
tarehe 4 mwezi huu Jeshi la Ethiopia llilianza mashambulizi dhidi ya Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray (The Tigray People's Liberation Front (TPLF)).
Hujuma hiyo imeanza kwa amri ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed.
Tigray ni eneo la jamii ya wachache lakini wenye nguvu ambao kwa miongo kadhaa wamekuwa wakiongoza muungano tawala nchini Ethiopia.
Miaka miwili nyuma na baada ya kuingia madarakani Abiy Ahmed, kuliundwa muungano mpya wa utawala ambao umesusiwa na jamii ya watu wa Tigray.