Ethiopia yatetea oparesheni za kijeshi Tigray, yasema lengo ni kuokoa taifa
Ethiopia imetetea operesheni ya kijeshi inayoendelea katika sehemu ya kaskazini mwa nchi hiyo na kusema oparesheni hiyo inalenga kuokoa taifa.
Akizungumza na waandishi habari, Redwan Hussein ambaye ni msemaji wa Kikosi cha Hali ya Dharura cha Taifa kilichoanzishwa kwa ajili ya Tigray amesema lengo la kuanzishwa kwa oparesheni ya kijeshi kaskazini mwa nchi hiyo wiki iliyopita ni kuiokoa nchi, mamlaka ya nchi na kuhakikisha nchi inashikamana pamoja. Amesema serikali iko tayari kukaa chini na kufanya mazungumzo na yeyote mwenye ugomvi na serikali.
Jeshi la Ethiopia tarehe 4 mwezi huu wa Novemba lilianzisha mashambulizi dhidi ya Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray (The Tigray People's Liberation Front (TPLF)). Hujuma hiyo ilianza kwa amri ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed. Taarifa zinasema Ethiopia imetumia ndege za kivita kudondosha mabomu katika eneo hilo ambalo linataka kujitenga.
Hussein amesema chama cha TPLF kimepora silaha nzito kutoka jeshini, ambapo serikali inalenga kuhakikisha silaha hizo hazitumiki dhidi ya Waethiopia na watu walio nje ya Ethiopia.
Amesema serikali imetangaza kukamata roketi na makombora yenye uwezo wa kwenda kilomita 300, ambapo TPLF nayo imesema haina uwezo wa kushambulia shabaha iliyo umbali wa kilomita 300 tu, bali pia inaweza kushambulia mji mkuu wa nchi hiyo Addis Ababa ambao upo umbali wa kilomita 700.
Waziri Mkuu Abiy Ahmed amesema serikali yake imejaribu kuepuka vita na mapigano lakini jambo hilo haliwezi kufanywa na upande mmoja. Waziri Mkuu wa Ethiopia amesema kuwa hujuma ya harakati ya Ukombozi wa Tigray dhidi ya kambi ya jeshi imevuka mistari myekundu. Abiy Ahmed pia amewataka Waethiopia kufuatilia hali ya mambo kwa utulivu na kushirikiana na jeshi la taifa.
Mzozo huo wa serikali ya Ethiopia na jimbo lake la kaskazini la Tigray umevuka mpaka baada ya maelfu ya watu kuhamia nchini Sudan, pamoja na wanajeshi walioasi. Karibu wakimbizi 6000 wakiwemo wanawake na watoto wamewasili katika mkoa wa Kassala nchini Sudan, na wengine wako njiani. Duru zinadokeza kuwa, zaidi ya Waethiopia 200,000 wanatarajiwa kuvuka mpaka na kuingia Sudan katika siku chache zijazo.
Wakati huo huo Umoja wa Afrika ametoa wito kwa Ethiopia kusitisha oparesheni yake ya kijeshi katika eneo la Tigray. Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ametoa wito wa usitishwaji wa mapigano huku akitaka pande zote hasimu zilinde na kuheshimu haki za raia.