Kabuga afikishwa katika Mahakama ya Umoja wa Mataifa, asema hana hatia
Mshukiwa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, Felicien Kabuga jana Jumatano alifikishwa katika Mahakama ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania ambapo alisisitiza kuwa hana hatia katika mashitaka ya jinai yanayomkabili.
Wakili wake, Emmanuel Altit aliiambia mahakama kuwa, mteja wake 'amechoka' na 'anafadhilisha asizungumze' wakati alipoulizwa na Jaji Lain Bonomy iwapo mshukiwa huyo mwenye zaidi ya miaka 80 yuko tayari kujibu mashitaka au la.
Altit amesema kimya cha mteja wake mahakamani hapo kinaashiria kuwa anaitakidi kuwa hana hatia katika mashitaka yote yanayomuadama yakiwemo ya mauaji na jinai dhidi ya binadamu.
Mbali na Jaji Bonomy raia wa Scotland, majaji wengine wanaosikiliza kesi ya Kabuga ni Graciela Susana Gatti Santana wa Uruguay na Mganda Elizabeth Ibanda - Nahamya.
Mwezi uliopita wa Oktoba, Mahakama ya Rufaa nchini Ufaransa ilikubali kumpeleka Kabuga kushtakiwa katika Mahakama ya Umoja wa Mataifa yenye makao yake mjini Arusha Tanzania, ambalo ni tawi la Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya ICC iliyoko Hague, Uholanzi.
Félicien Kabuga, mmoja wa watuhumiwa wakuu wa mauaji ya kimbari ya Rwanda yaliyotokea mwaka 1994 alikamatwa katika mji wa Paris nchini Ufaransa mwezi Mei mwaka huu baada ya kuishi kwa kujificha kwa muda wa miaka 26.
Mauaji ya kimbari ya Rwanda yalitokea kwa muda wa siku 100 kuanzia Aprili 6 mwaka 1994 baada ya Rais Juvenal Habyarimana na mwenzake wa Burundi Cyprien Ntaryamira, wote Wahutu, kupoteza maisha wakati ndege yao ilipotunguliwa katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali.
Shambulizi hilo lilipelekea wanajeshi wa Kihutu wa serikali na wanamgambo waitifaki waliokuwa na misimamo mikali kuanzisha mauaji ya kimbari kwa lengo la kuwaangamiza Watutsi waliokuwa wachache ambapo watu 800,000 waliuawa katika mauaji hayo.