Mgogoro wa Ethiopia washadidi huku viwanja vya ndege vikishambuliwa
Mzozo unaoendelea nchini Ethiopia unaonekana kuchukua mkondo mpana zaidi baada ya maeneo kadhaa ya viwanja vya ndege kushambuliwa na wapiganaji wa Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray (The Tigray People's Liberation Front (TPLF) kaskazini mwa nchi hiyo.
Taarifa zaidi zinasema, wapiganaji hao wa jimbo la kaskazini mwa Ethiopia la Tigray wamefyatua maroketi katika jimbo jirani na mengine kutua katika mji mkuu wa nchi jirani ya Eritrea katika mzozo wao na serikali ya Ethiopia unaoendelea kupanuka.
Hali ya uhasama baina ya serikali na Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray, ilishadidi zaidi mwezi huu na kusababisha makabiliano ya kijeshi.
Maafisa wamesema "maeneo ya viwanja vya ndege " yameharibiwa katika shambulio la maroketi. Waasi hao wamethibitisha kuhusika, wakisema kuwa mashambulio yalikuwa ni ya ulipizaji kisasi.
Wakati huo huo, Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet, ameonya kuwa madai ya mauaji nchini Ethiopia, ikiwa yatathibitishwa, yatakuwa uhalifu wa kivita.
Onyo hilo linakuja baada ya shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International kuripoti kwamba, makumi ya raia waliuawa katika jimbo la Tigray.
Michelle Bachelet anataka uchunguzi kamili ufanyike na amesema wale waliohusika na makosa hayo iwapo yatathibitishwa lazima wawajibishwe.
Mamlaka husika katika jimbo la Tigray zimekanusha madai kwamba vikosi vya jimbo la Tigray vilitekeleza mauaji hayo. Bi Bachelet amebaini kwamba kipaumbele cha kwanza ni kumaliza mapigano.
Kwa upande wake Umoja wa Mataifa una wasiwasi kwamba mzozo huo unaweza kuongezeka na hata kuenea mbali na mipaka ya Ethiopia. Tayari maelfu ya watu wameyatoroka makazi yao na kukimbilia nchini Sudan kutokana na mapigano yanayoendelea.