Mgogoro wa Ethiopia; Tigray yaendelea kuwa kitovu cha mzozo
Mgogoro ulioibuka nchini Ethiopia umekuwa ukichukua mkondo mpana zaidi siku baada ya siku.
Makumi ya watu katika jimbo la Tigray wameuawa huku maelfu ya wengine wakiwa katika hali ya kukimbilia nchi jirani. Tayari maelfu ya raia wanaripotiwa kuwasili katika nchi jirani na Ethiopia wakikwepa mapigano yanayoendelea nchini kwao kati ya jeshi la serikali na Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray (The Tigray People's Liberation Front (TPLF) kaskazini mwa nchi hiyo. Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusiana na madai ya kufanyika mauaji makubwa dhidi ya raia katika jimbo la Tigray.
Ethiopia ni nchi ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya watu barani Afrika ambapo ina wakazi zaidi ya milioni 100. Kabla ya hapo Ethiopia ilikuwa ikitambulika kama kigezo cha 'kurejea katika demokrasia'.
Hata hivyo kuanzia tarehe 4 ya mwezi huu wa Novemba kumekuwa kukishuhudiwa vitendo vya utumiaji mabavu katika uhusiano wa serikali kuu ya Addis Ababa inayoongozwa na Waziri Mkuu Abiy Ahmed na jimbo la Tigray la kaskazini mwa nchi hiyo. Wakazi wa jimbo la Tigray wanaunda asilimia 6 ya idadi ya wananchi wa Ethiopia. Tigray ni eneo la jamii ya wachache lakini wenye nguvu ambao katika miaka 30 iliyopita wamekuwa wakiongoza muungano tawala nchini Ethiopia. Lakini mwaka 2018 Abiy Ahmed, anayetoka katika kaumu ya Oromo alifanikiwa kushika hatamu za uongozi akiwa Waziri Mkuu.
Baada ya kuingia madarakani Abiy Ahmed aliunganisha muungano tawala na kuwa chama kimoja. Hata hivyo Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray ambayo kwa miaka mingi ilikuwa katika muuungano huo tawala ilikataa kujiunga na chama kipya.
Hivi karibuni Bunge la Ethiopia lilipasisha kwa wingi wa kura mchakato wa kubadilisha muundo wa nguvu za utekelezaji huko Tigray baada ya kuibuba mapigano baina ya harakati hiyo na wanajeshi wa serikali kuu. Uamuzi huo ulitathminiwa na jimbo la Tigray kwamba, ni hatua nyingine yenye lengo la kuiweka kando harakati ya eneo hilo katika muundo wa kisiasa wa Ethiopia. Viongozi wa Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray na akthari ya wananchi wa eneo hilo wanaamini kuwa, serikali kuu wa Etthiopia haiheshimu maslahi ya eneo hilo. Ni kutokana na sababu hiyo, ndio maana mielekeo ya kujitenga imepata nguvu baina ya wananchi wa eneo hilo.
Hivi sasa baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kutoa amri ya kushambuliwa wanamgambo wa Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray kivitendo ametangaza vita dhidi ya harakati hiyo. Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa ujumbe akieleza wasiwasi alionao kuhusiana na matukio ya Tigray kaskazini mwa Ethiopia na kutoa wito wa kusitisha mara moja mapigano hayo sambamba na kutoa fursa ya kuanza kutafutwa njia za amani za kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo.
Mzozo unaoendelea nchini Ethiopia unaonekana kuchukua mkondo mpana zaidi baada ya maeneo kadhaa ya viwanja vya ndege kushambuliwa na wapiganaji wa Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray (The Tigray People's Liberation Front (TPLF) kaskazini mwa nchi hiyo. Wapiganaji hao Tigray wamefyatua maroketi katika jimbo jirani na mengine kutua katika mji mkuu wa nchi jirani ya Eritrea katika mzozo wao na serikali ya Ethiopia unaoendelea kupanuka. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, hivi sasa Ethiopia inaelekea kuingia katika vita vya ndani.
Hapana shaka kuwa kuendelea vita nchini Ethiopia bila kujali vinatokana na taathira kutoka nje au ndani, ni jambo ambalo linaweza kuwa na taathira hasi kwa sehemu kubwa ya bara la Afrika na kuvuruga amani na uthabitri wa moja ya maeneo ya kistratejia ulimwenguni. Kwa muktadha huo, inaonekana kuwa, kupatikana utatuzi kwa ajili ya mazunguumzo ya amani ili kuhitimisha mzozo huo, ni jambo ambalo linaweza kumpatia itibari nyingine Abi Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia ambaye ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel.