Nov 18, 2020 11:58 UTC
  • Kongo DR yatangaza kumalizika janga la Ebola nchini humo

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza habari ya kudhibitiwa mlipuko wa 11 wa ugonjwa wa Ebola nchini humo, ambao umesababisha vifo vya watu 55 tangu mwezi Juni mwaka huu hadi sasa.

Dakta Eteni Longondo, Waziri wa Afya wa DRC ametangaza hayo na kuongeza kuwa, nchi hiyo imefanikiwa kudhibiti janga la Ebola kwa kuwa hakuna kesi yoyote mpya ya ugonjwa huo iliyoripotiwa kwa muda wa siku 50 zilizopita.

Ameeleza bayana kuwa, katika mlipuko huo wa 11 wa ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika kipindi cha miaka 44, watu 138 wameambukizwa maradhi hayo huku wengine 55 wakifariki dunia.

Mwezi uliopita wa Oktoba, Dakta Jean Jacques Muyembe, mtaalamu wa vijidudu maradhi anayehusika na mapambano ya kuzuia maambukizi ya Ebola nchini Kongo DR alitangaza kuwa, hali ya maambukizi ya ugonjwa huo katika maeneo ya kaskazini magharibi mwa nchi hiyo imedhibitiwa na hakuna ripoti iliyotolewa kwa siku 16 mtawalia kuhusu kesi yoyote mpya ya maradhi hayo.

Maafisa wa afya wa DRC wakipeana chanjo ya Ebola

Katika mlipuko huo wa 11 wa Ebola nchini DRC uliotangazwa tarehe Mosi Juni mwaka huu wa 2020, wagonjwa wa awali walibainika kwenye mji mkuu wa jimbo la Ikweta, Mbandaka na kisha ugonjwa huo ukasambaa katika maeneo mengine ya nchi.

Mlipuko wa 10 wa maambukizi ya virusi vya Ebola ulioanza mwezi Mei mwaka 2018 kaskazini magharibi mwa nchi hiyo na kudhibitiwa kikamilifu mwezi Juni mwaka huu, ulisababisha vifo vya watu wasiopungua 2,277. 

  

 

Tags