Umoja wa Mataifa umetaka kusaidiwa kupatiwa ufumbuzi maafa ya kibinadamu nchini Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i64763-umoja_wa_mataifa_umetaka_kusaidiwa_kupatiwa_ufumbuzi_maafa_ya_kibinadamu_nchini_ethiopia
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka kutekelzwa jitihada za upatanishi huko Ethiopia na kufunguliwa korido za misaada ya kibinadamu nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 21, 2020 08:46 UTC
  • Umoja wa Mataifa umetaka kusaidiwa kupatiwa ufumbuzi maafa ya kibinadamu nchini Ethiopia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka kutekelzwa jitihada za upatanishi huko Ethiopia na kufunguliwa korido za misaada ya kibinadamu nchini humo.

Akizungumza na vyombo vya habari mjini New York Marekani Antonio Guterres ameeleza kusikitishwa na hatua ya viongozi wa Ethiopia ya kukataa kukubali jitihada za upatanishi kutoka nje ya nchi hiyo na kufunguliwa korido za misaada ya kibinadamu ili kuwasaidia raia wanaotaabika na mapigano yanayoendelea katika eneo la Tigray nchini humo. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aidha amesema kuwa ana wasiwasi na hali ya mambo ya sasa huko Ethiopia pamoja na taathira mbaya za hali ya kibinadamu iliyojitokeza katika nchi hiyo na huko Sudan; na kusisitiza juu ya udharura wa kutekelezwa juhudi ili kukusanya misaada ya kibinadamu kwa ajili ya raia wa nchi hizo. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa bila ya kuashiria eneo husika ameongeza kuwa na hapa ninamnukuu: "Sisi tunataka kuheshimiwa kikamilifu sheria za kimataifa na kufunguliwa korido za kibinadamu." 

Guterres pia amesisitiza kuwa, kuna haja ya kuuungwa mkono kila juhudi na ubunifu wa Umoja wa Afrika (AU) wenye lengo la kuyapatia ufumbuzi maafa ya kibinadamu huko Ethiopia.  

Hadi sasa maelfu ya watu wameuliwa na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa katika mapigano katika eneo la Tigray kati ya Harakati ya wapiganaji wa TPLF na wanajeshi wa serikali kuu ya Ethiopia. Abiy Ahmed Waziri Mkuu wa Ethiopia tarehe 4 mwezi huu wa Novemba alitoa amri ya kutekelezwa mashambulizi katika eneo la Tigray baada ya kuwatuhumu wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray kuwa wamevishambulia vikosi vya jeshi la nchi hiyo.

Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia