Ethiopia yawaeleza wajumbe wa AU: Hatutafanya mazungumzo yoyote na viongozi wa Tigray
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesisitiza kwa mara nyingine kuwa hatofanya mazungumzo na viongozi wa eneo lililoasi la Tigray.
Abiy ametoa sisitizo hilo katika mazungumzo na wajumbe watatu wa Umoja wa Afrika AU.
Amewaambia wajumbe hao wa AU wanaojaribu kuhitimisha mgogoro wa mapigano kati ya jeshi la Ethiopia na vikosi vya eneo la Tigray kwamba yuko tayari kuzungumza na wale aliowaita wawakilishi "wanaoendesha mambo kisheria" katika eneo hilo.
Mazungumzo baina ya Waziri Mkuu wa Ethiopia na wajumbe wa Umoja wa Afrika yalifanyika jana Ijumaa huku watu wakiendelea kuukimbia mji mkuu wa eneo la Trigray Makelle kwa kuhofia mashambulio makali baada ya Abiy kutangaza siku ya Alkhamisi kuanza kile alichokiita "awamu ya mwisho" ya shambulio la majuma matatu lililoanzishwa na jeshi la serikali kuu ya Addis Ababa.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu huyo wa Ethiopia baada ya mazungumzo ya kiongozi huyo na wajumbe wa AU imesema, serikali inawahakikishia raia katika eneo la Tigray kuwa itawapa ulinzi na usalama.
Hakukuwa na kauli yoyote iliyotolewa na wajumbe wa Umoja wa Afrika baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia hiyo jana, ambao ni rais wa zamani wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, rais wa zamani wa Msumbiji Joaquim Chissano na rais wa zamani wa Afrika Kusini Kgalema Motlanthe.
Msemaji wa Umoja wa Afrika Ebba Kalondo hajaeleza kama wajumbe hao wa umoja huo watakutana pia na viongozi wa eneo la Tigray, wazo ambalo limepingwa na ofisi ya Abiy.
Serikali ya Addis Ababa ilikuwa imewapatia wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) inyaoendesha eneo hilo la kaskazini mwa Ethiopia muhula wa hadi Jumatano iliyopita wawe wameweka chini silaha au mji wa Makelle ambao ni makao makuu ya eneo hilo wenye watu wapatao laki tano ushambuliwe kijeshi.
Imekuwa vigumu kuelewa kinachoendelea hivi sasa katika eneo la Tigray baada ya mawasiliano ya simu na intaneti kukatwa na kuwepo udhibiti mkali wa kufika katika eneo hilo. Hata hivyo wanadiplomasia wawili wamenukuliwa wakisema, mapigano yamepamba moto katika maeneo kadhaa nje ya mji wa Mekelle.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ambaye ndiye aliyekuwa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel mwaka uliopita wa 2019 amekataa pia kile alichokiita "uingiliaji" wa kimataifa katika mgogoro wa serikali yake na eneo la Tigray.../