Ethiopia yaruhusu UN ifikikishe misaada Tigray bila vizingiti
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i64972-ethiopia_yaruhusu_un_ifikikishe_misaada_tigray_bila_vizingiti
Ethiopia imetoa idhini kwa Umoja wa Mataifa kupeleka misaada bila vizingiti katika jimbo la kaskazini la Tigray, kufuatia wiki kadhaa za kuishawishi ifanye hivyo wakati operesheni za kijeshi zikiendelea.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 03, 2020 01:00 UTC
  • Ethiopia yaruhusu UN ifikikishe misaada Tigray bila vizingiti

Ethiopia imetoa idhini kwa Umoja wa Mataifa kupeleka misaada bila vizingiti katika jimbo la kaskazini la Tigray, kufuatia wiki kadhaa za kuishawishi ifanye hivyo wakati operesheni za kijeshi zikiendelea.

Makubaliano hayo, yaliyosainiwa na waziri wa amani wa Ethiopia, yanaruhusu utoaji wa misaada ya kiutu na huduma kwa wakazi walioko hatarini katika maeneo yanayoshikiliwa na serikali jimboni Tigray na maeneo jirani ya Amhara na Afar. Waziri Mkuu Abiy Ahmed alianzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya wapiganaji wa Ukombozi wa Watu wa Tigray - TPLF Novemba 4 akiwalaumu kwa kufanya mashambulizi kwenye vituo vya jeshi la serikali. Serikali ilikata mawasiliano ya simu na intaneti katika eneo hilo na kuzuia usafiri wa kuingia Tigray, hali iliyofanya kuwa vigumu kutathmini mazingira ya eneo hilo.

Waziri Mkuu  wa  Ethiopia Abiy Ahmed

Karibu watu 600,000 wanaoishi Tigray walitegemea msaada wa chakula kabla ya mapigano kuanza, wakiwemo wakimbizi 96,000 wa Kieritrea. Umoja wa Mataifa unasema kuna uhaba wa chakula, mafuta na fedha.

Hayo yanajiri wakati ambao Kiongozi wa chama cha TPLF amesema askari wake wanaendelea kupambana na jeshi la serikali, siku mbili baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kutangaza ushindi katika eneo hilo.