Ripoti: Ethiopia huenda ikakumbwa na janga kubwa la kibinadamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i65041-ripoti_ethiopia_huenda_ikakumbwa_na_janga_kubwa_la_kibinadamu
Ripoti ndefu iliyotolewa na Shirika la Habari la Associated Press inaeleza kuwa, Ethiopia huenda ikakumbwa na janga kubwa la kibinadamu endapo vita vinavyoshuhudiwa katika jimbo la Tigray vitaendelea.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 06, 2020 08:22 UTC
  • Ripoti: Ethiopia huenda ikakumbwa na janga kubwa la kibinadamu

Ripoti ndefu iliyotolewa na Shirika la Habari la Associated Press inaeleza kuwa, Ethiopia huenda ikakumbwa na janga kubwa la kibinadamu endapo vita vinavyoshuhudiwa katika jimbo la Tigray vitaendelea.

Ripoti hiyo inabainisha kwamba, maafa hayo yatajumuisha maafa ya kibinadamu na sekta ya afya na kwamba, yatakuwa makubwa kuwahi kushuhudiwa katika eneo hilo.

Kdhalika ripoti ya shirika hilo inasema kuwa, maafa hayo yatakuwa makubwa hasa kwa kutilia maanani kwamba, hivi sas Ethiopia inakumbwa na tatizo la kuenea virusi vya Corona na maradhi mengine hali ambayo imeifanya sekta ya afya kukabiliwa na changamoto kubwa.

Aidha asasi mbalimbali za kieneo na kimtaifa zimetahadharisha kuhusiana na kuibuka maafa ya kibinadamu katika jimbo la Tigray endapo vita hivyo havitakomeshwa kwani bado kuna shida ya ufikishaji misaada katika eneo hilo licha ya kufikiwa makubaliano baina ya serikali ya Addis Ababa na Umoja wa Mataifa kuhusiana na suala hilo.

 

Jeshi la Ethiopia 

 

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wameziambia duru za habari kwamba, hawakuweza kufikisha misaada kama walivyokubaliana na serikali ya Addis Ababa, hasa kwenye maeneo ambayo yanadhibitiwa na vikosi vya serikali.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, serikali ya Ethiopia imetangaza kuwa, imewakamata mateka na kuwaua akthari ya viongozi wa waasi wa Harakati ya Ukombozi wa Wananchi wa Tigray.

Tarehe 4 mwezi uliopita wa Novemba na baada ya kuvituhumu vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray kwamba vimewashambulia askari wa jeshi la serikali, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alitoa amri ya kushambuliwa kijeshi eneo hilo la Tigray.