TPLF: Mapigano yangali yanaendelea katika eneo la Tigray
Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray TPLF imesema mapigano yangali yanaendelea kati yake na jeshi la serikali kuu ya Ethiopia katika eneo hilo.
TPLF imetangaza kuwa mapigano hayo yanaendelea nje ya mji wa Mekelle, makao makuu ya eneo la Tigray.
Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray TPLF vilevile imewatuhumu askari wa jeshi la serikali kuwa wamehusika na uporaji na kuripua kwa mabomu maeneo mbalimbali ya mji wa Mekelle.
Jeshi la serikali kuu ya Ethiopia kwa upande wake limetangaza kuwa, limebakiza siku chache tu kabla ya kuwakamata viongozi wa vikosi vya waasi na kwamba mapigano yanakaribia kumalizika baada ya kupita wiki moja tangu lilipoudhibiti mji wa Mekelle.
Umoja wa Mataifa umesema una wasiwasi juu ya hali ya eneo la Tigray licha ya jeshi la serikali kuu ya Ethiopia kujitangazia ushindi katika mapigano na vikosi vya Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray ya kulidhibiti eneo hilo.
Eneo la Tigray lililoko kaskazini ya Ethiopia limeshuhudia mapigano katika wiki za karibuni kati ya jeshi la nchi hiyo na vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray TPLF.
Serikali ya Adds Ababa, ambayo inaituhumu TPLF kuwa inataka kulitenganisha eneo la Tigray na ardhi ya Ethiopia, limetangaza hivi karibuni kuwa vikosi vya jeshi vimeudhibiti mji wa Makelle, makao makuu ya eneo hilo.
Habari zilizoripotiwa kutoka Tigray zinaeleza kuwa mauaji ya kiholela ya mamia ya watu yamefanywa katika eneo hilo wakati wa mapigano baina ya pande mbili za jeshi la serikali na vikosi vya TPLF.../