Askari wa Ethiopia waua waasi 370 eneo la Oromia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i65127-askari_wa_ethiopia_waua_waasi_370_eneo_la_oromia
Vikosi vya usalama nchini Ethiopia vimewaua waasi 370 katika oparesheni kali iliyofanyika katika mkoa wa Oromia, katikati ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 11, 2020 03:38 UTC
  • Askari wa Ethiopia waua waasi 370 eneo la Oromia

Vikosi vya usalama nchini Ethiopia vimewaua waasi 370 katika oparesheni kali iliyofanyika katika mkoa wa Oromia, katikati ya nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa Alhamisi na ofisa mahusiano wa Polisi mkoa wa Oromia, inasema waasi 370 wameuawa na wengine 330 wamekamatwa kwenye operesheni ya usalama iliyodumu kwa mwezi mmoja.

Hali kadhila taarifa hiyo imesema waasi hao wanaaminika kuwa wafuasi wa kundi la OLA (Oromo Liberation Army) ambalo limejitenga na kundi jingine la waasi linalojulikana kama OPLA (Oromo Liberation Front)

Kundi hilo la OLA linakadiriwa kuwa na wapiganaji wapatao 2,800 kwenye sehemu za magharibi na kusini mwa mkoa wa Oromia.

Makundi ya waasi katika eneo hilo yanadai kupigania haki za Waoromo ambao ni asilimia 35 ya watu milioni 110 wa Ethiopia.

Baina ya mwezi Juni na Julai mwaka huu, watu zaidi ya 240 waliripotiwa kuuawa nchini Ethiopia, baada ya ghasia kuibuka kufuatia kifo cha mwanamuziki maarufu  wa kabila la Oromo, Hachalu Hundessa.

Hachalu alizikwa Julai 2 nyumbani kwake Ambo, katikati ya mkoa wa Oromia huku kukiwa na ulinzi mkali. Wafuasi wake waliuona muziki wake kuwa uliotetea haki za watu wa kabila la Oromo, ambao kwa muda mrefu walijihisi kutengwa na serikali.

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alisema mauaji ya Hachalu pamoja na maandamano ya baada ya kifo hicho yalikuwa sehemu ya mpango wa kuzusha machafuko nchini humo.

Oparesheni hiyo ya usalama ya serikali ya Ethiopia katika eneo la Oromia inajiri wakati ambao eneo la Tigray nchini humo nalo linakumbwa na uasi unaoongozwa na kundi la TPLF ambalo karibuni hivi lilipata pigo kubwa kutoka kwa jeshi la serikali.