Mripuko wa bomu waua na kujeruhi kadhaa nchini Ethiopia
(last modified Mon, 21 Dec 2020 08:22:48 GMT )
Dec 21, 2020 08:22 UTC
  • Mripuko wa bomu waua na kujeruhi kadhaa nchini Ethiopia

Kwa akali watu watatu wameuawa na wengine watano wamejeruhiwa baada ya bomu 'lililotelekezwa' kuripuka katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Mripuko huo ulijiri jana Jumapili katika eneo la Lideta lililoko viungani wa Addis Ababa. Kamanda wa Polisi katika eneo hilo, Alemayehu Ayalke ameliambia shirika la habari la serikali la EBC kuwa, waliouawa katika mripuko huo wa bomu ni watu wasio na makazi na wanaoshi mitaani.

Hakuna kitu chochote kinachoashiria kuwa mripuko huo una mfungamano na mgogoro unaoendelea kushuhudiwa katika eneo la Tigray, kaskazini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Serikali imesema uchunguzi wa kubaini chanzo cha mripuko huo umeanza na kwamba wananchi watapatiwa taarifa ya kina kuhusu mkasa huo pale uchunguzi utakapomalizika.

Mapigano ya ndani katika eneo la Tigray

Eneo la Tigray lililoko kaskazini ya Ethiopia limeshuhudia mapigano katika wiki za karibuni kati ya jeshi la nchi hiyo na vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray (TPLF).

Serikali ya Addis Ababa, ambayo inaituhumu TPLF kuwa inataka kulitenganisha eneo la Tigray na ardhi ya Ethiopia, ilitangaza hivi karibuni kuwa vikosi vya jeshi vimeudhibiti mji wa Mek’ele, ambao ni makao makuu ya eneo hilo. Mapigano hayo yamesababisha watu 50,000 wakimbilie katika nchi jirani ya Sudan.