Zaidi ya watu 100 wauawa katika mapigano Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i65362-zaidi_ya_watu_100_wauawa_katika_mapigano_ethiopia
Watu zaidi ya 100 wameuawa katika hujuma iliyotekelezwa na watu wasiojulikana huko Ethiopia katika eneo la Benishangul-Gumuz.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 23, 2020 23:59 UTC
  • Zaidi ya watu 100 wauawa katika mapigano Ethiopia

Watu zaidi ya 100 wameuawa katika hujuma iliyotekelezwa na watu wasiojulikana huko Ethiopia katika eneo la Benishangul-Gumuz.

Kwa mujibu wa Tume ya Haki za Binadamu Ethopia watu hao wameuawa katika kijiji cha Bekoji katika wilaya ya Bulen.

Duru zinadokeza kuwa wanamgambo waliwashambulia wakazi wakiwa wamelala mapema Jumatano ambapo mbali na watu 100 kuuawa wengine kadhaa pia wamejeruhiwa.

Eneo hilo ni makazi ya makabila kadhaa likiwemo kabila la Gumuz. Hatahivyo katika miaka ya hivi karibuni wakulima na wafanya biashara kutoka eneo jirani la Amhara wamehamia eneo hilo na kupelekea watu wa kabila la Gumuz kulalamika kuwa ardhi yao yenye rotuba imeporwa.

Hivi sasa baadhi ya viongozi wa kabila la Amhara wanasema ardhi katika eneo hilo, hasa ukanda wa Metekel ni milki yao, madai ambayo yanakanushwa vikali na Wagumuz wanaosema wao ni wenyeji wa eneo hilo.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Mashambulizi hayo yamekuja siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, mkuu wa jeshi na maafisa wengine kutembelea eneo hilo na kutoa wito wa kuwepo utulivu baada ya mapigano makali baina ya makabila mbali mbali katika miezi ya hivi karibuni. Mwezi uliopita watu 34 waliuawa baada ya basi kushambuliwa.

Katika ujumbe wa Twitter Jumatano, Waziri Mkuu Abiy alisema maadui wanalenga kuigawa Ethiopia kwa misingi ya kikabila na kidini lakini hawataruhusiwa kufanya hivyo.

Hayo yanajiri huku Jeshi la Ethiopia likiendeleza oparesehni katika eneo la Tigray kukabiliana na waasi.

Tokea Abiy Ahmed aingia madarakani mwaka 2018, Ethiopia imekuwa ikikabiliwa na machafuko ya kikabilia katika majimbo kadhaa nchini humo.