Waliofariki katika shambulio la watu wenye silaha magharibi ya Ethiopia wafika 207
Tume ya Haki za Binadamu ya Ethiopia imetangaza kuwa shambulio lililofanywa na watu wenye silaha magharibi mwa nchi hiyo limesababisha watu 207 kuuawa.
Tume ya Haki za Binadamu ya Ethiopia EHRC, ambayo katika ripoti yake ya awali ilitangaza kuwa watu zaidi ya 100 waliuawa katika shambulio hilo, ilieleza katika taarifa iliyotoa jana Jumamosi kuwa, idadi ya waliouawa katika shambulio hilo lililofanywa na watu wenye silaha magharibi mwa nchi hiyo imefika watu 207.
EHRC aidha imeeleza kwamba, juhudi zinaendelea kufanywa ili kuwatambua waathirika wa shambulio hilo na kuweza kuwasaidia jamaa zao walionusurika baada ya kupata hati na vitambulisho vyao. Kwa mujibu wa ripoti ya tume hiyo ya haki za binadamu ya Ethiopia, watu 133 miongoni mwa waliouawa ni wanaume na waliosalia ni wanawake, watoto na wazee.
Kwa mara nyingine tena Tume ya Haki za Binadamu ya Ethiopia imerudia mwito na ombi lake la kutaka itumwe haraka misaada ya kibinadamu katika eneo hilo na kueleza wasiwasi ilionao kuhusu hali za idadi ya wakimbizi waliotokana na mapigano ya karibuni nchini humo.
Siku ya Jumatano iliyopita, watu wenye silaha walishambulia mji wa Bulen magharibi mwa Ethiopia wakati watu wa mji huo walipokuwa wamelala na kuchoma moto nyumba zao.
Katika wiki za karibuni, Ethiopia imekumbwa na matukio kadhaa, kubwa zaidi likiwa ni la vita kati ya jeshi la serikali na vikosi vya eneo la Tigray.../