Ethiopia yapokea vizuri juhudi za kupunguza ugomvi kati yake na Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i65962-ethiopia_yapokea_vizuri_juhudi_za_kupunguza_ugomvi_kati_yake_na_sudan
Wizara ya Mambo ya Nje ya ya Ethiopia imetangaza kuwa Addis Ababa inakaribisha na imepokea vizuri juhudi za kupunguza ugomvi na wasiwasi kati yake na jirani yake Sudan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 22, 2021 00:26 UTC
  • Ethiopia yapokea vizuri juhudi za kupunguza ugomvi kati yake na Sudan

Wizara ya Mambo ya Nje ya ya Ethiopia imetangaza kuwa Addis Ababa inakaribisha na imepokea vizuri juhudi za kupunguza ugomvi na wasiwasi kati yake na jirani yake Sudan.

Mtandao wa habari wa al Nashra umenukuu taarifa ya jana Alkhamisi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia ikisema kuwa, Addis Ababa itaendelea na juhudi zake za kuleta amani na utulivu kati yake na Sudan. Taarifa ya wizara hiyo pia imesema, wananchi wa nchi mbili za Ethiopia na Sudan ni ndugu na udugu wao ni wa jadi, wa kale na wa kidamu ambao hauwezi kuvunjika.

Taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia imetolea siku chache baada ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abi Ahmed kuoinya vikali Sudan na kusisitiza kwamba msimamo wa Addis Ababa mbele ya Khartoum si ishara ya udhaifu.

Mkoa wa Qaradif wa Sudan ambako Ethiopia inadai raia wake wananyanyaswa

 

Ugomvi katika eneo la mapakani baina ya Sudan na Ethiopia umezidi kuwa mkubwa tangu mwanzoni mwa mwezi Novemba 2020 wakati Ethiopia ilipoendesha operesheni za kijeshi za kuwang'oa waasi wa eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia. Vita hivyo vimepelekea zaidi ya wakimbizi 50 elfu wa Ethiopia wakimbilie mashariki mwa Sudan.

Ugomvi mkubwa uliopo baina ya Addis Ababa na Khartoum ni mashamba ya kilimo katika eneo la al Fushqa mkoani Qadarif mashariki mwa Sudan. Tangu takriban miaka 26 iliyopita, wanamgambo wa Ethiopia walilivamia eneo hilo, wakawafukuza wakulima wa Sudan na kulikalia kwa mabavu.

Sudan inaituhumu Ethiopia kuwa inawaunga mkono wanamgambo hao. Addis Ababa inakanusha madai hayo.

Hata hivyo, Ethiopia imekasirishwa mno na uamuzi wa Sudan wa kuendesha operesheni za kuwafurusha wanamgambo hao katika eneo lake hilo.