Magaidi 15 wa al-Shabaab wauawa katika operesheni ya jeshi la Somalia
Wanamgambo 15 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wameangamizwa katika operesheni ya jeshi la Somalia kusini mwa nchi.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, wanachama hao wameangamizwa katika shambulio la anga lililofanywa na wanajeshi wa Somalia na washirika wao, dhidi ya kambi ya mazoezi ya genge hilo katika mkoa wa Lower Juba, yapata kilomita 12 kutoka eneo la Jamame.
Kadhalika vikosi jeshi la Somalia vikishirikiana na vikosi vya jimbo la Kusini Magharibi vimefanikiwa kuwatia mbaroni wanachama wanne wa al-Shabaab katika eneo la Udinli, mkoa wa Bai.
Haya yanajiri huku kamanda mashuhuri wa kundi hilo la kigaidi ambaye jina lake halikutajwa akijisalimisha kwa vyombo vya usalama katika mji wa Baadwayn.
Wiki iliyopita, vikosi vya jeshi hilo vilifanikiwa kuwaangamiza wanamgambo 52 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab katika operesheni ya shambulio iliyofanywa dhidi ya ngome ya kundi hilo katika eneo la Shabelle ya Chini kusini mwa nchi hiyo.
Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabaab limekuwa likiendesha kampeni ya mtutu wa bunduki kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya Somalia.